Hatimaye Uingereza imejiondoa rasmi kutoka Muungano wa Ulaya (EU) baada ya kuwa mwanachama kwa miaka 47.
Hatua hiyo ya kihistoria ambayo ilifanyika saa sita usiku saa za Uingereza iliadhimishwa kwa sherehe ambazo zilianza kufanyika katika kumbi tofauti za burudani huku watu wakisubiri saa iliyowekwa ya nchi hiyo kujiondoa rasmi EU.
Mishumaa iliwashwa kuadhimisha siku hiyo huko Scotland, mamia ya watu walikusanyika katika bustani ya bunge kusherehekea Brexit, wakiimba nyimbo za kizalendo na kushangilia hutuba kutoka kwa viongozi wakuu walioshinikiza nchi kujiondoa katika muungano wa Ulaya (EU), akiwemo Nigel Farage.
Kiongozi huyo wa chama cha Brexit alisema: “Naomba tusherehekee usiku huu jinsi ambavyo hatujawahi kufanya hivyo tena.
Waziri Mkuu wa Uingereza Boris Johnson katika ujumbe kwenye mtandao wa kijamii saa moja kabla ya Uingereza kujiondoa, alisema “kwa watu wengi hii ni hatua ya matumaini,na pia kuna wale ambao wameghadhabishwa na kuingiwa na hofu kuhusu hali ya baadae”
“Na kuna kundi la tatu pengine kubwa zaidi ambalo lilikua limeanza kuwa na wasiwasi kuhusu mgogoro wa kisiasa na kuhofia hautawahi kufika kikomo, naelewa hisia zote hizo na jukumu letu kama serikali, sasa ni kuleta nchi hii pamoja na kuendelea mbele.” Amesema waziri Johnson
Hata hivyo raia wa Uingereza wanatarajiwa kushuhudia mabadiliko kidogo yanayoanza moja kwa moja kwasababu nchi hiyo imejiondoa kwenye muungano wa Ulaya.
Serikali ya Uingereza inalenga kutia saini makubaliano ya biashara huru na Umoja wa Ulaya, Lakini viongozi wa Ulaya wameonya kwamba Uingereza inakibarua kigumu cha kufikia makubalino ndani ya siku ya ukomo iliyotengwa.