‘Safari ya matumaini’ iliyoanzishwa na mbunge wa Monduli , waziri mkuu wa zamani, Edward Lowassa na kuishia kwenye mlango wa Kamati ya Usalama na Maadili ya Chama Cha Mapinduzi imepata muelekeao mwingine na kuhamia Chadema.

Hayo yamebainishwa hivi karibuni na mbunge wa Arusha Mjini, Kamanda wa Chadema, Godbless Lema alipokuwa akiwahutubia wananchi katika jimbo la Monduli ambapo aliwapokea madiwani 20 kutoka Chama Cha Mapinduzi waliotangaza kukihama chama hicho wakipinga utaratibu uliotumika kuliondoa jina la Edward Lowassa katika kinyang’anyiro cha kumsaka mgombea urais.

Lema aliuambia umma uliohudhuria katika tukio hilo kuwa viongozi wa safari ya matumaini wanatarajiwa kutangaza hivi karibuni kuihama CCM na kuhamia Chadema.

Kauli ya Lema imeongeza nguvu ya tetesi kuwa Edward Lowassa na kambi yake wanafanya mazungumzo na Chadema na Ukawa ili kupata nafasi ya kugombea urais kupitia umoja huo huku ikielezwa kuwa kumekuwa na mvutano mkali kati ya mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na Katibu Mkuu wa chama hicho, Dr. Wilbroad Slaa kuhusu ombi hilo.

Ukawa inayoundwa na Chadema, NCCR – Mageuzi na Chama cha Wananchi (CUF) imeendelea kuwasubirisha wananchi wanaotaka kufahamu hatima ya mpango wao wakumsimamisha mgombea wa mmoja katika nafasi ya urais na kugawana majimbo.

Ester Bulaya Aimwaga CCM
#MTVMAMA Vijembe Vyatawala Pongezi Za Tuzo Ya Diamond, Dole La Kati Aliloonesha Lawasha Moto