Baada ya kuonyesha kiwango cha chini kila anapopewa nafasi hivi karibuni, inavyoonekana sasa maisha ya mshambuliaji Laudit Mavugo ndani ya Simba yanaelekea mwishoni.
Simba kwa sasa ipo nchini Djibouti kucheza dhidi ya Gendarmerie Nationale katika Kombe la Shirikisho ukiwa ni mchezo wa pili baada ya awali Simba kupata ushindi wa mabao 4-0 kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar.
Katika msafara huo wa kwenda nchini Djibouti, mshambuliaji Laudit Mavugo amebaki Dar huku nahodha John Bocco ambaye afya yake ilikuwa na utata, aliondoka kuongozana na wenzake katika safari hiyo.
Akizungumza juu ya kuachwa kwa Mavugo licha ya kuwa fiti kiafya, Ofisa Habari wa Klabu ya Simba, Haji Manara amesema kuwa kuna tatizo katika usajili wa Mavugo kwenye michuano ya kimataifa.
Manara hakufafanua juu ya tatizo hilo la usajili lakini kwa kuwa Simbaa ilikamilisha michakato yake mapema kuhusu usajili wa kimataifa huku Mavugo akiwa mmoja wa wachezaji waliokuwepo klabuni hapo kwa muda mrefu, dalili zinaonyesha wazi hana umuhimu kikosini.
Wakati wa dirisha dogo ilielezwa kuwa mchezaji huyo alikuwa miongoni mwa wanaotakiwa kufungashiwa virago lakini ilishindikana kutokana na sababu kadhaa za ndani ya klabu.
Hivyo, kwa mwenendo huo huku kiwango chake kikiwa kimeshuka, ni wazi safari ya Mavugo imewadia hasa kwa kuwa Emmanuel Okwi na John Bocco wamekuwa na makali katika kucheka na nyavu.