Safari ya kiungo mshambuliaji wa klabu ya Simba Said Hamisi Ndemla imesogezwa mbele na sasa anatarajiwa kuondoka kesho kuelekea nchini Sweden kwa ajili ya kufanya majaribio kwenye klabu ya ya AFC Eskilstuna.

Ndemla alitarajiwa kuondoka leo, kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana na idara ya habari na mawasilino ya klabu ya Simba, lakini leo mchana idara hiyo inayoongozwa na  Hajji Sunday Manara imeeleza kuwa, mabadiliko hayo hayataathiri muda wake wa majaribio katika klabu hiyo, ambao ni siku 14.

Taarifa ya jana ilieleza; “Klabu inaamini Ndemla atafanya vizuri na kufuzu katika majaribio hayo, na kama itakuwa tofauti na hivyo, mchezaji huyo ataendelea kuichezea Simba. Huu ni utaratibu wa klabu wa kuwapa nafasi wachezaji wake kwenda nje kujaribu bahati zao za kucheza soka ya kulipwa,”.

Akifanikiwa kufuzu majaribio katika klabu hiyo, Ndemla mwenye umri wa miaka 21 ataungana na Mtanzania mwingine, mshambuliaji Thomas Ulimwengu, ambaye hata hivyo kwa sasa ni majeruhi anasumbuliwa na maumivu ya goti tangu Septemba, mwaka huu na atakuwa nje hadi Januari mwakani.

Ndemla aliibukia kikosi cha timu ya vijana ya Simba, maarufu kama Simba B mwaka 2012 kabla ya kupandishwa timu ya wakubwa mwaka 2013 na tangu mwaka 2015 amekuwa kwenye kikosi cha timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars.

Mbwana Samatta kuikosa Benin
Moyes alamba shavu West Ham