Mabingwa wa Soka la Wanawake Tanzania Bara ‘Simba Queens’ wanatarajia kuondoka Dar es salaam leo Jumanne (Oktoba 25), kuelekea Rabat-Morocco, tayari kwa Mshike Mshike wa Klabu Bingwa Afrika utakaoanza Oktoba 30.
Simba Queens imepata nafasi ya kushiriki Michuano ya Klabu Bingwa Afrika kwa Wanawake, baada ya kutawazwa kuwa Mabingwa wa Afrika Mashariki na Kati ‘CECAFA’ mwezi Agosti, wakiifunga She Corporate ya Uganda.
Meneja wa Simba Queens Seleman Errasy Makanya amesema kikosi chao kinatarajia kuondoka leo usiku na kitawasili Morocco kesho Jumatano (Oktoba 26).
“Tunatarajia kuondoka Oktoba 25 usiku na tutaingia Morocco kesho Jumatano (Oktoba 26), tunaamini tutakuwa na muda mzuri wa kukamilisha maandalizi yetu kabla ya kuanza kupambana mwishoni mwa juma hili.” amesema Makanya
Katika Michuano ya Klabu Bingwa Afrika kwa Wanawake Simba Queens imepangwa ‘Kundi A’ na wenyeji AS FAR (Morocco), Green Buffaloes (Zambia) na Determine Girls (Liberia).
Simba Queens itaanza Kampeni ya kusaka taji la Afrika Oktoba 30 kwa kucheza na wenyeji AS FAR (Morocco), kwenye Uwanja wa Moulay Hassan, mjini Rabat.
Mabingwa Watetezi Mamelodi Sundowns (Afrika Kusini) wamepangwa ‘Kundi B’ sambasamba na timu za Bayelsa Queens (Nigeria), Wadi Degla (Misri) na TP Mazembe (DR Congo).