Wakati Droo ya makundi ya kuwania kufuzu Fainali za Kombe la Dunia 2026, katika nchi za Marekani, Canada na Mexico ikichezeshwa leo Alhamis (Julai 13) kwa upande wa Bara la Afrika, Taifa Stars ina uwezekano mkubwa wa kufuzu ikiwa itachanga vyema karata zake.
Uongozi wa kundi ambalo itapangwa katika Droo hiyo itakayochezeshwa jijini Abidjan, Ivory Coast, utaifanya Stars ikate moja kwa moja tiketi ya kuiwakilisha Afrika katika fainali hizo za kihistoria, ambazo kwa mara ya kwanza idadi ya timu shiriki itakuwa 48, huku Afrika ikiwa na nafasi tisa moja kwa moja.
Lakini kama itamaliza katika nafasi ya pili, na ikawa miongoni mwa timu nne zilizovuna alama nyingi katika nafasi hiyo, itacheza mechi za mchujo kusaka nafasi moja ya mchujo dhidi ya timu kutoka bara jingine, ambayo itapangwa nayo.
Katika Droo ya leo itakayochezeshwa kuanzia saa 1 usiku, Stars itakuwa katika chungu cha nne na timu moja kutoka hapo itapangwa na nyingine moja kutoka katika chungu cha kwanza, moja kutoka chungu cha pili, timu moja ya chungu cha tatu, nyingine moja kutoka katika chungu cha nne, na moja moja kutoka chungu cha tano na sita.
Timu za chungu cha kwanza ambazo mojawapo ni lazima ipangwe na Taifa Stars ni Morocco, Senegal, Tunisia, Algeria, Misri, Nigeria, Cameroon, Mali na Ivory Coast, wakati timu zilizopo katika chungu cha pili ni Burkina Faso, Ghana, Afrika Kusini, Cape Verde, DR Congo, Guinea, Gabon, Guinea ya Ikweta na Zambia.
Katika chungu cha tatu kuna timu za Uganda, Benin, Mauritania, Kenya, Congo, Madagascar, Namibia, Guinea Bissau na Angola wakati chungu cha nne ambacho Tanzania ipo kina timu pia za Msumbiji, Malawi, Gambia, Sierra Leone, Togo, Zimbabwe, Afrika ya Kati na Libya.
Mratibu wa timu za taifa za Tanzania, Danny Msangi amesema wanaisubiria kwa hamu Droo hiyo kufahamu watapangwa na timu zipi kwenye kundi moja, lakini ndoto yao ni kucheza Kombe la Dunia 2026.
“Tunafahamu makundi hayatokuwa na timu rahisi, kwanza tunasubiri kujua timu za kundi letu, kisha tuanze mikakati, ndoto na hamu yetu ni kucheza fainali za Kombe la Dunia,” amesema Msangi.