Serikali kurejesha safari za ndege kutoka Tanzania kwenda nchini India kuanzia leo Agosti 29, 2021 ni baada ya kusimama kwa muda tangu mwezi Mei 2021 ikiwa ni mkakati wa kukabiliana na maambukizi ya Uviko-19
Hayo yamesemwa na Msemaji wa Serikali, Gerson Msigwa wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma ambapo amesema kwamba safari hizo zitaanza mapema leo huku Serikali ikiendelea kujipanga kufungua maeneo mengine.
Msigwa amesema wakati wowote kuanzia sasa Serikali itafungua safari za Nairobi nchini Kenya.
“Tumefungua milango ya safari za ndege, kutoka na kuingia Tanzania lakini tumepunguza gharama za vipimo ikiwemo kipimo cha lazima cha Uviko-19 kutoka Dola 25 hadi Dola 10 kwa wanaopita mipakani, lakini kwa mipaka ya nchi jirani imekuwa bure,” amesema Msigwa.
Msigwa amesema wameendelea kufanya maboresho makubwa ikiwemo kuagiza ndege mpya nyingine tano ambazo tayari zimelipiwa malipo ya awali na zinatarajia kuletwa nchini 2023.
Kwa mujibu wa Msigwa, ndege zinazonunuliwa ni pamoja na ndege kubwa ya mizigo na ndege za abiria.