Kampuni kubwa zaidi ya mtandao wa simu za mkononi nchini Kenya ya Safaricom imejibu tuhuma zilizoelekezwa kwake na aliyekuwa mgombea urais akiungwa mkono na ngome ya NASA, Raila Odinga kuwa walihusika kuharibu matokeo ya uchaguzi mkuu nchini humo.

Akizungumza katika mahojiano maalum na shirika la habari la Reuters, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Safaricom, Bob Collymore amesema kuwa hawakuhusika na makosa yoyote yaliyofanyika na kwamba walichokifanya wao ni kuhakikisha wanatoa huduma ya uhakika ya mfumo wa mtandao kama walivyokubaliana na wateja wao ambao ni tume ya uchaguzi ya IEBC.

Collymore amesema kuwa kama NASA wana malalamiko yoyote juu yao wanapaswa kwenda mahakamani ambapo Safaricom wataenda kujitetea dhidi ya tuhuma hizo.

Ofisa Mtendaji Mkuu wa Safaricom (Kenya), Bob Collymore

Raila aliwatuhumu baadhi ya maafisa wa Safaricom akidai kuwa walishirikiana na maafisa wasio waaminifu wa IEBC kufanya uchakachuaji kupitia mfumo wa kutuma matokeo (Kenya Integrated Elections Management Systems kits) kwa lengo la kumsaidia Rais Uhuru Kenyatta kupata ushindi.

Raila aliwaagiza wanasheria wa NASA kuanza mchakato wa kuwafikisha mahakamani baadhi ya wafanyakazi wa Safaricom ambao walihusika katika vitendo hivyo.

Mahakama ya Juu nchini humo ilibatilisha matokeo ya uchaguzi yaliyotangazwa na IEBC, yaliyompa ushindi wa asilimia 54 Rais Uhuru Kenyatta.

Mahakama hiyo iliamuru uchaguzi mwingine kufanyika baada ya siku 60 kwa mujibu wa Katiba ya nchi hiyo.

Kichuya aanza mazoezi chini ya uangalizi
Mwanamke wa kwanza Marekani ahitimu mafunzo ya ‘ukomando’ ardhini