Shabiki Maarufu wa klabu ya Simba SC Said Muchacho amesema hana shaka na mchezo wa kesho Jumamosi (April 30), kwani anakiamini kikosi chake kwa kusema kinakwenda kuibuka na ushindi dhidi ya Simba SC.
Muchacho ambaye ni muasisi za Kundi wa KIDEDEA ambalo lilitamba miaka ya 1990-2000 amesema Simba SC ina kikosi bora, na ina kila sababu ya kuibuka na ushindi dhidi ya Young Africans, japo mchezo huo wakati mwingine huwa na matokeo ya kushangaza.
Amesema anafahamu hata mashabiki wa Young Africans wanamini timu yao itashinda dhidi ya Simba SC, na suala hilo limekua kawaida, lakini kwake hawezi kuipa nafasi timu pinzani kushinda dhidi ya timu yake.
“Hizi DABI kila mwaka huwa zinakuwepo mara mbili, ikitokea kwenye Kombe la Shirikisho basi ni bahati tu, lakini kwa mchezo kama wa kesho lazima kila mwaka uwepo, sasa mimi sina wasiwasi wowote kwa sababu ninaamini kikosi changu kina ubora kuliko kile cha wenzetu.”
“Japo mchezo huu huwa na matokeo ya ajabu sana, iliwahi kutokea Young Africans wanaongoza mabao 3-0 kipindi cha kwanza na mimi niliudhuka nikaondoka Uwanjani, lakini kipindi cha pili Simba SC ilisawazisha na mchezo ukamalizika kwa 3-3.”
“Kuna wakati hata sisi Simba SC tuliwahi kuongoza mabao 2-0, wenzetu wakaja wakasawazisha mchezo ukamalizika kwa sare ya 2-2, hivyo mchezo huu huwa na maajabu sana.” amesema Muchacho
Katika hatua nyingine Shabiki huyo wa Simba SC amewataka wachezaji wa timu zote mbili kucheza kwa uungwana kwenye mchezo wa kesho ili wasiumizane, kwa sababu msimu ujao watakua na jukumu zito la kuiwakilisha Tanzania kimataifa.
“Niwaombe wachezaji wote wawe makini sana, wasicheze mchezo wa ajabu, wanapaswa kucheza kwa uungwana, wasiumizane, msimu ujao unafahamu tena timu hizi zinakwenda kuliwakilisha taifa la Tanzania Kimataifa, ila ninasisitiza nina imani timu yangu inakwenda kushinda.” ameongeza Muchacho.
Young Africans kesho itaingia Uwanja wa Benjamin Mkapa huku ikiwa inaongoza msimamo wa Ligi Kuu kwa kufikisha alama 54 ambazo zinawapa nafasi kubwa ya kutwaa ubingwa wa Tanzania Bara msimu huu 2021/22.
Simba SC inayotetea ubingwa inashika nafasi ya pili kwenye msimamo huo, ikiwa na alama 41, ambazo zinaifanya kuwa nyuma kwa alama 13 dhidi ya Young Africans.