Kiungo wa Simba SC anayecheza Mtibwa Sugar kwa mkopo Said Khamis Ndemla, ameomba radhi kwa kitendo cha kinyama alichomfanyia Kiungo Sadio Kanoute, wakati wa mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara jana Alhamis (Juni 23), Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam.
Ndemla alioneshwa kadi nyekundu kwa kosa la kumkanyaga kwa makusudi sehemu ya paja Kanoute, aliyekua kwenye harakati za kuokoa mpira uliokuwa unaelekea langoni mwa Simba SC.
Kiungo huyo mzawa ametumia muda wake kuandika ujumbe wa kuomba radhi kupitia ukurasa wake wa Instagram, ambao umeonesha anajutia kosa alilolifanya.
“…Ninafahamu sana kwamba kujutia nilichofanya na kuomba msamaha hakutabadilisha au kufuta kusimamishwa, lakini ni vyema kujua jinsi ya kujifunza kutokana na makosa yako … ningependa kuchukua nafasi hii kuwasilisha msamaha wangu wa dhati kutoka moyoni mwangu kwa kaka yangu Sadio Kanoute, timu ya Simba na mashabiki!
Aidha, napenda kuwaomba radhi wachezaji wenzangu na mashabiki wa soka kwa ujumla. Siwezi kuficha kiwango ambacho nimewakatisha tamaa. Nisameheni sana ?” Ameandika Ndemla
Katika mchezo huo Simba SC iliibuka na ushindi wa mabao 2-0, yakifungwa na Pappe Ousmane Sakho na Mlinda Lango Shaban Kado aliyejifunga.
Kwa ushindi huo Simba SC imefikisha alama 60 zinazoendelea kuiweka nafasi ya pili katika msimamo wa Ligi Kuu, ikitanguliwa na Young Africans yenye alama 70 kileleni.
Mtibwa Sugar yenye alama 31, imeendelea kushika nafasi ya 12 ikisaliwa na michezo miwili dhidi ya Namungo FC Uwanja wa Manungu Complex mkoani Morogoro, kisha itamaliza msimu kwa kucheza na Young Africans Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam.
Simba SC itamaliza michezo yake ugenini dhidi ya Tanzania Prisons katika Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya na kisha watapambana na Mbeya Kwanza FC kwenye Uwanja wa Majimaji mjini Songea mkoani Ruvuma.