Licha ya kuitwa mbele ya Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji ya Shirikisho la Soka nchini Tanzania ‘TFF’, Sintofahamu imeendelea kutawala kati ya Kiungo kutoka visiwani Zanzibar Feisal Salum Abdallah ‘Fei Toto’ dhidi ya Uongozi wa Young Africans.
Pande hizo mbili zilifika mbele ya Kamati hiyo, baada ya Uongozi wa Young Africans kumshitaki ‘Fei Toto’ kwa kosa la kutoroka kambini na kuvunja Mkataba kinyume na utaratibu.
Saa kadhaa baada ya kikao kuchukua nafasi yake katika viunga na Shirikisho la Soka nchini Tanzania ‘TFF’ Fei Toto’ na Meneja wake walitoka katika chumba maalum, ambacho kilikuwa na kazi ya kumaliza sintofahamu baina ya pande hizo mbili.
Hata hivyo Meneja wa ‘Fei Toto’ ambaye jina lake halikupatikana kwa haraka alizungumza na baadhi ya vyombo vya habari na kusema bado kuna wingu zito limetanda katika Sintofahamu hiyo.
Meneja huyo amesema kubwa linaloendelea baina yao na Uongozi wa Young Africans na mchezaji wake ni kutokuelewana na ameshindwa kutoa maelezo ya kina kama mchezaji wake atarejea kwa Wananchi.
“Bado kuna wingu zito limetanda, hakuna hata mwanga, ninaamini maelewani yatapatina japo siwezi kufahamu kama Fei Toto atarudi Young Africans.”
“Kuhusu wapi atakapocheza mchezaji wangu siwezi kusema lolote kwa sasa, TFF watatangaza maamuzi kwa sababu wao ndio wenye mpira wao.” amesema Meneja
Wakati huo huo Fai toto amekataa katakata kuzungumzia lilikuwa likiendelea katika Chumba kilichosikiliza sakata lake, huku akisisitiza kumshukuru mwenyezi mungu.
Desemba 23-2022 zilitoka taarifa za Fei toto kuandika Barua ya kuvunja Mkataba wake ndani ya Klabu ya Young Africans, ambapo tangu hapo hajaonekana kambini akitimkia kwao Zanzibar kabla ya hivi karibuni kusafiri kwenda Dubai kwa mapumziko.