Uongozi wa Klabu ya Simba SC umebisha hodi Shirikisho la Soka Duniani ‘FIFA’ ukilitaka kutoa ridhaa ya kumruhusu Mshambuliaji kutoka Jamhuri ya Afrika ya Kati  Ceser Lobi Manzoki, ambaye anadaiwa kuzuiwa na viongozi wa Klabu bingwa nchini Uganda Vipers SC.

Manzoki anayedaiwa kumalizana na Simba SC, amezuiwa nchini Uganda kwa madai bado ana mkataba na Klabu ya Vipers SC, ambao utafikia kikomo mwezi Oktoba mwaka huu.

Taarifa kutoka Simba SC zinaeleza kuwa Vipers SC wamesisitiza kuhitaji kiasi cha Shilingi Milioni 100 ili kumuachia Mshambuliaji huyo, ambaye tayari ameshaonesha nia ya kutaka kucheza katika Ligi ya Tanzania Bara.

Inadaiwa kuwa Uongozi wa Simba SC umefanya maamuzi ya kwenda FIFA kwa kufuata taratibu zote, ili kufanikisha suala la kumnasa Manzoki, kwa ajili ya kumtumia msimu ujao wa Ligi Kuu na Michuano ya Kimataifa.

“Manzoki ni mchezaji ambaye Simba SC tayari imeshamalizana naye, amesaini mkataba wa miaka miwili, changamoto iliopo kwa Vipers, wamegoma kumuachia wakidai kabakiza miezi miwili kwenye mkataba wake na wametuambia tutoe Shilingi Milioni 100, kitu ambacho hakiwezekani,” amesema mmoja wa Wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi Simba SC

Kwa upande wa Afisa Mtendaji Mkuu wa Simba SC Barbara Gonzalez amesema walishamaliza zoezi zima la usajili, ambapo kuna wachezaji watatu wa kigeni wanaosubiri tu kutambulishwa, huku taarifa zikidai kuwa katika majina hayo yupo Manzoki.

“Wanasimba wasiwe na wasiwasi juu ya usajili tayari tumeshamaliza kusajili na kuna wachezaji watatu watatambulishwa hivi karibuni, kila kitu tumekifanya kwa umakini sana.” Amesema Mtendaji huyo

Fiston Mayele aichimba mkwara Simba SC
Simba SC yaahidi kurudisha furaha 2022/23