Sakata la kupingwa kwa mkataba wa kampuni ya SportPesa limechukua sura mpya, baada ya mwenyekiti wa baraza la wadhamini wa klabu ya Simba SC Hamis Kilomoni kudai hakushirikishwa.
Kilomoni ambaye amekuwa na misimamo ya kutaka kuona Simba SC haiingii kwenye mpango wa malumbano kati ya wanachama na viongozi wa ngazi za juu, amezungumza na Dar24 na kudai suala la kusainiwa kwa mkataba huo wa miaka mitano wenye thamani ya shilingi billion 4.9 halikumfikia kabla na baada ya kusaniwa.
Amesema taarifa hizo amekuwa akiziona na kuzisikia katika vyombo vya habari tangu siku ya jumamosi, na jambo kubwa analolifanya sasa ni kuzungumza na mjumbe mwenzake wa baraza la wadhamini wa klabu ya Simba Ramesh Patel, ili kufahamu kama alishirikishwa katika mpango huo.
“Sifahamu lolote kuhusu huo mkataba, hata mimi nimekua naziona hizo taarifa tangu siku ya jumamosi, lakini kiukweli sijashirikishwa kwa hatua yoyote ile, ninachokifanya sasa ni kuwasiliana na mwenzangu ili nifahamu kama alishiriki katika harakati za mazungumzo na hiyo kampuni ambayo inasemekana wameidhamini Simba SC,” alisema.
“Kwa sasa mimi ni mgonjwa, na wakati mwingi ninakua nyumbani nimepumzika, na ilikua vyema kwa viongozi wa klabu ya Simba kuja kuzungumza na mimi ili kufahamu njia ya kupita kuliko kufanya hayo ambayo ninayaona katika vyombo vya habari.” Kilomoni aliiambia Dar24.
Simba SC imeingia katika hali ya taharuki baada ya kusainiwa kwa mkataba wa kampuni ya SportPesa yenye makao makuu nchini Kenya, huku ikielezwa mwanachama Mohamed Dewji “Mo” ambaye alikua na mpango wa kutaka kuwekeza klabuni hapo kwa mfumo wa hisa akiudai uongozi kiasi cha shilingi billion 1.4, ambacho kimetumika kama malipo ya mishahara ya wachezaji kwa makubaliano maalum.
Mbali na “Mo”, mapema jana kulikua na taarifa za kujiuzulu kwa mjumbe wa kamati ya utendaji ya klabu ya Simba Zachariah Hans Pope, lakini baadae alitengua maamuzi yake na kuamua kurejea kundini.