Kaimu Katibu Mkuu wa Young Africans, Wakili Simon Patrick amesema Kiungo Mshambuliaji wa klabu hiyo, Bernard Morrison hakusafiri kuelekea Shinyanga na Dodoma kucheza michezo ya Ligi Kuu Tanzania Bara kwa sababu ya majeraha yaliyokuwa yakimkabili na sio vinginevyo kama baadhi ya watu wanavyozusha.
Patrick ambaye amekaimu nafasi ya katibu mkuu klabuni hapo baada ya kujiuzulu kwa Dk. David Luhago siku mbili zilizopita, amesema alipata majeraha ya kidole cha mguu akiwa katika mchezo wa kirafiki dhidi ya Transit Camp, kabla ya kuendelea kwa Ligi kuu Tanzania Bara mwishoni mwa juma lililopita.
“Morrison alicheza ile mechi yetu ya kirafiki dhidi ya Transit Camp ambayo walimchezea sana rafu akawa ameumia kidole chake. Kwenye hicho kidole kucha ikawa kama imetoka. Hivyo nimekutana naye kujua hali yake na kumuelekeza taratibu za kufuata na ameelewa na ameomba radhi kwa hiyo ataungana na wenzake tarehe 18,” amesema Wakili Patrick.
Patrick amesema kuwa, ukiondoa majeraha hakuna tatizo lingine lolote baina ya Morrison na klabu hiyo na mchezaji ana furaha ndani ya timu.
Sakata la Morrison kutosafiri na timu kwenda katika mikoa ya Shinyanga ambako Young Africans ilicheza na Mwadui FC mwishoni mwa juma lililopita na kuibuka na ushindi wa bao 1-0 na pia Dodoma ambako leo itacheza dhidi ya JKT Tanzania, lilipamba moto baada ya kuwepo na taarifa tofauti kutoka ndani ya klabu hiyo juu ya kutosafiri kwake.
Hata hivyo Kocha wa Young Africans, Luc Eymael jana alitangaza msimamo wake kwa kumtaka Morrison kuwaomba radhi wachezaji wenzake, benchi la ufundi, mashabiki, wanachama pamoja na viongozi na wadhamini wa klabu hiyo.
Kocha huyo kutoka nchini Ubelgiji alisisitiza kwamba, Morrison pamoja na mchezaji yoyote wa Young Africans lazima ajue kwamba kila kitu anachokifanya ni kama timu na huku akionya kuwa hakuna mchezaji nyota asiyepata msaada uwanjani kutoka kwa wenzake.
Alimtaka Morrison kujua kuwa hakuna mchezaji nyota duniani anayecheza mpira peke yake uwanjani bila msaada wa wengine, “hata ukiwachukua kina Cristiano Ronaldo wawili, Messi wawili na Sergio Ramos wawili wacheze dhidi ya wachezaji 11, lazima watafungwa. Timu ni mchango wa watu wengi.
“Najua Morrison kwa sasa ndiye mchezaji nyota wa Yanga, hilo halina ubishi, lakini lazima ajue kuwa umaarufu wake unatokana na msaada au ushirikiano na wachezaji wengine hilo ni jambo muhimu kujua, Yanga ni timu na wala si ya mchezaji mmoja pekee.”