Kiungo Mshambuliaji kutoka nchini Senegal Pape Ousman Sakho amesema hana shaka na mpango wa kucheza hatua ya Robo Fainali ya Kombe la Shirikisho Barani Afrika, baada ya kikosi cha Simba SC kupoteza dhidi ya ASEC Mimosas Jumapili (Machi 20).
Simba SC ilipoteza ugenini kwa kufungwa 3-0 mjini Cotonou-Benin, hatua ambayo inaifanya klabu hiyo ya Dar es salaam kusubiri hadi kwenye mchezo wa mwisho ili kufahamu hatma yake ya kufuzu hatua ya Robo Fainali.
Sakho amesema Simba SC ina kikosi imara na chenye kupambana bila hofu, hivyo anaamini kwenye mchezo wa mwisho wa ‘Kundi D’ dhidi ya USGN itakua na nafasi ya kushinda na kutimiza lengo la kutinga Robo Fainali.
“Simba SC ni timu kubwa na ina kikosi bora, tunaweza kupata alama tatu katika uwanja wowote ndani na nje ya Afrika, sina shaka na mchezo wetu wa mwisho dhidi ya USGN ninaamini tutashinda”
“Ninajua hata wapinzani wetu watakua na nia ya kuja kushinda katika Uwanja wetu wa nyumbani, lakini niwafahamishe kuwa Dar es salaam haitakua sehemu rafiki kwao kupata matokeo zaidi ya kuondoka na hasara ya kupoteza.” amesema Sakho
Simba SC itacheza dhidi ya USGN Uwanja wa Benjamin Mkapa April 03, huku ASEC Mimosas ikisafiri kuelekea mjini Berkane-Morocco kupambana na RS Berkane.
Msimamo wa ‘Kundi D’ hadi sasa ASEC mimosas inaongoza ikiwa na alama 09, ikifuatiwa na RS Berkane yenye alama 07 sawa na Simba SC huku USGN ikiburuza mkia kwa kuwa na alama 05.