Jina la mshambuliaji wa Misri, Mohamed Salah limeteka mada ya mechi kati ya timu hiyo ya Afrika na wenyeji Urusi itakayoshuhudiwa leo.
Kocha Mkuu wa Urusi, Stanislav Cherchesov ametumia muda mwingi kama ilivyokuwa kwa wengine katika mkutano wake na waandishi wa habari kwenye uwanja wa Krestovsky kuhusu mechi hiyo, kueleza kuwa kikosi chake kitamdhibiti Salah ambaye anatarajiwa kucheza kwa mara ya kwanza kwenye fainali hizo baada ya kuukosa mchezo kati ya timu yake na Uruguay.
“Niseme nini? Ninaiamini timu yangu. Ninawaamini wachezaji wangu na nitawapa jibu rahisi,” alisema na kuongeza kuwa wako tayari kuendeleza heshima waliyoizoa ya 5-1 dhidi Saudi Arabia kwenye mechi ya ufunguzi.
Naye golikipa wa Urusi ambaye pia ni nahodha wa kikosi hicho, Igor Akinfeev alionesha kuchoshwa na maswali kuhusu Salah na kisha kueleza kuwa anaamini hawatacheza na midoli.
“Tunajua kuwa hakutakuwa na midoli inayocheza dhidi yetu. Utakuwa mchezo wa viumbe hai. Sio Mo Salah pekee atakayekuwa akicheza dhidi yetu. Kuna wachezaji wengine zaidi ya 20. Tutaona kitakachotokea,” alisema.
Afya ya Salah ilikuwa kitendawili kufuatia majeraha ya bega aliyoyapata katika mechi ya fainali ya mabingwa kati ya timu yake ya Liverpool dhidi ya Real Madrid.
Ingawa Shirikisho la Mpira wa Miguu la Misri lilitangaza kuwa Salah alikuwa tayari kushiriki mechi ya kwanza ya timu hiyo katika kundi A dhidi ya Uruguay, kocha Hector Cuper aliamua kutompanga ili asimuweke hatarini mchezaji huyo ambaye ni hazina ya kutegemewa, mchezo uliomalizika kwa kipigo cha 1-0.
Leo ni leo, Misri na Senegal zinakuwa timu mbili za Afrika zitakazoingia uwanjani kusaka nafasi ya ushindi. Wakati Misri watakuwa wakicheza mechi yake ya pili dhidi ya wenyeji Urusi, Senegal watafungua dimba dhidi mapema dhidi ya Poland kwenye mchezo wa Kundi H.