Katibu Mkuu wa zamani wa  Umoja wa Nchi za Afrika (O.A.U) ambayo sasa ni Umoja wa Afrika (A.U), Dk. Salim Ahmed Salim amekosoa uamuzi wa kutangazwa kwa marudio ya uchaguzi Zanzibar.

Dk. Salim ameeleza kuwa Jumuiya za Kimataifa zinashangaa uamuzi wa kufutwa kwa uchaguzi wa Zanzibar ili hali ripoti za waangalizi wa kimataifa zilionesha kuusifia uchaguzi huo kuwa ulifanyika kwa uwazi na haki huku ukitawaliwa na amani na utulivu.

“Ni hatua ambayo imewashangaza wengi…imeibua sintofahamu kubwa katika nchi yetu kwa sababu uchaguzi uliopita Tanzania ilipata sifa, baada ya uchaguzi kufanyika kwa amani na utulivu. Lakini kitendo cha kufutwa kumewashangaza wengi na bado suala hili halieleweki,” alisema.
 
“Pia hili jambo sidhani kama ni la mtu mmoja…sidhani kama ni la Jecha peke yake. Huu si mustakabali mzuri kabisa, Zanzibar ni nchi ndogo, lakini ina historia kubwa kisiasa hivyo juhudi za pamoja zifanyike kutatua mgogoro huu kwa matakwa ya Watanzania kwa ujumla,” aliongeza.
Dk. Salim ambaye aliwahi kuwa Waziri Mkuu alitoa wito kwa viongozi wote kuendelea kuhimiza amani na utulivu pamoja na kuendelea na majidiliano ya kutafuta maridhiano ya amani hata kama tarehe ya marudio ya uchaguzi imeshatangazwa na Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC), Jecha Salim Jecha.

“Nchi ipo katika hali mbaya, migogoro iko kila pahala,Watanzania hatujazoea. Jambo hili la Zanzibar likiendelea litazaa matatizo makubwa katika Taifa letu. “Waliangalie kwa uzito hata kama tarehe ya uchaguzi imetangazwa waendelee na mazungumzo,” alisema.

Akieleza kama suala la Zanzibar liliwahi kujadiliwa katika vikao vya Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi ambayo yeye pia ni mjumbe, Dk. Salim alieleza kuwa jambo hilo liliwahi kugusiwa lakini halikujadiliwa na kutolewa maamuzi.
Mwenyekiti wa ZEC ameitangaza hivi karibuni kuwa uchaguzi wa Zanzibar utarudiwa Machi 20 mwaka huu na hakutakuwa na kampeni wala mabadiliko ya wagombea.

Walichozungumza Lowassa na Maalim Seif walipojifungia Dodoma
Kanye West amalizana na hili, adai amefunika wote