Kamati ya waamuzi ya shirikisho la soka nchini TFF imeahidi kuwataja waamuzi watakaochezesha mchezo wa Simba na Yanga saa 24 zijazo.
Mwenyekiti wa kamati hiyo Salum Umande Chama amezungumza na mwandishi wetu na kusisitiza kuwataja waamuzi hao siku ya jumatano (Kesho).
Amesema kamati yake inaendelea kulifanyia kazi suala hilo zito na wanatambua shauku ya mashabiki wa klabu hizo kongwe ya kutaka kumfahamu mwamuzi atakaesimamia sheria za mchezo huo wa jumamosi.
“Kamati yangu ipo katika hatua za mwisho kabla ya kutangaza majina ya waamuzi watakaochezesha siku ya jumamosi, ninawataka wadau wa soka nchini kote kuwa wastahamilivu, tunaimani tutamtaja mwamuzi wenye vigezo vya kuumudu mchezo huo.”
“Umekua utamaduni kwa kamati yangu kumtangaza mwamuzi siku tatu kabla ya mchezo, hata ukifuatilia katika mchezo wa mzunguuko wa kwanza wa Simba na Yanga tulimtangaza Martin Saanya na wenzake siku tatu kabla.” Alisema Chama.
Hata hivyo Chama amewahusia mashabiki wa soka watakaokwenda uwanjani siku ya jumamosi kuwa na ustaarabu wa kuheshimu maamuzi ya mwamuzi, ili kutorudia makosa ya kuharibu miundombinu ya uwanja wa taifa.
“Tuache kwenda uwanjani tukiwa na matokeo yetu mifukoni, soka ni mchezo wa wazi kila kitu kitaonekana na kama itatokea mwamuzi ataboronda kamati yangu na mamlaka nyingine za soka zitaona na kuchukua hatua. Sio kufanya maamuzi ya kuharibu miundombinu ya uwanja wa Taifa.” Alisisitiza Chama.
Katika mchezo wa mzunguuko wa kwanza Simba na Yanga walitoka sare ya kufungana bao moja kwa moja.
Mwamuzi Martin Saanya alilalamikiwa kwa kuruhusu bao la Yanga lililofungwa na Amis Tambwe ambaye alidaiwa kuunawa mpira kabla ya kuukwamisha wavuni, hali ambayo ilisababisha mashabiki waliodhaniwa kuwa wa Simba kung’oa viti na kuvirusha uwanjani.
Tukio lingine ambalo liliwakera mashabiki wanaodaiwa kuwa wa Simba, ni hatua ya Mwamuzi wa pembeni (Mshika Kibendera) kukataa bao lililofungwa na Ibrahim Ajib kwa kudai alikua ameotea.