Aliyekua mshambuliaji wa klabu ya Atletico Madrid Salva Ballesta ameanza chochoko za kutaka kuona meneja wa sasa wa klabu hiyo Diego Simeone, anaondoka mwishoni mwa msimu huu.
Ballesta ameanzisha chochoko hizo, baada ya kusema anaamini kikosi cha Atletico Madrid kunaweza kuendelea kupambana bila ya kuwa na Simione.
Ballesta alisema maneno hayo alipohojiwa na gazeti la Marca, ambapo alisisitiza anaamini muda wa Simione kukaa klabuni hapo umekwisha kutokana na hali halisi inayoonekana uwanjani.
“Tunamshukuru sana Simeone kwa kazi nzuri aliyoifanya tangu alipokuwa meneja, lakini kwa hapa tulipofikia naamini kikosi kitakua na uwezo wa kuendelea kupambana bila ya Simione kwa msimu ujao.”
“Daima nitaendelea kuyakumbuka mazuri aliyoyaleta hapa, kwa sababu tumeona timu ilibadilika na ilipambana na kila klabu iliyokutana nayo hapa Hispania na hata nje ya hapa, lakini kwa mwenendo tulionao hivi sasa, hatuna budi kusaka mtu mwingine atakae endelea kufanya mazuri zaidi.” Alisema Ballesta.
Simeone anaendelea kuhusishwa na mpango wa kutimikia nchini Italia kujiunga na magangwe wa mjini Milan “Inter Milan”.
Atletico Madrid jana ilipoteza mchezo dhidi ya mabingwa watetezi wa ligi ya nchini Hispania FC Barcelona na inakamata nafasi ya nne kwenye msimamo wa ligi hiyo kwa kuwa na point 45 huku kinara Real Madrid akiongoza kwa point 55.