Nahodha na mshambuliaji wa Taifa Stars Mbwana Ally Samatta amethibitisha kupokea lawama zilizotolewa na baadhi ya mashabiki wa soka nchini, kupitia mitandao ya kijamii kuhusu kiwango alichokionyesha juzi, wakati wa mchezo wa pili wa kundi J wa kuwania kufuzu fainali za mataifa ya Afrika (AFCON 2021).
Samatta amethibitisha kupokea ujumbe wa baadhi ya mashabiki hao, kwa kuwajibu kupitia ukurasa wake wa mtandao wa Twitter, akiwa safarini kurejea nchini Ubelgiji, kuendelea na majukumu ya kuitumikia klabu yake ya KRC Genk.
Samatta alilazimika kuondoka moja moja kurejea Ubelgiji akitokea Tunisia ulipochezwa mchezo wa pili wa kundi J dhidi ya Libya, ambao walichomoza na ushindi wa mabao mawili kwa moja.
Hata hivyo baada ya mchezo huo Sammata aligoma kuzungumzia suala la tuhuma alizotupiwa na baadhi ya mashabiki, kwa kusema “Sio jambo jema kuzungumzia nimecheza vipi, lakini yatupasa kutambua tumepoteza mchezo, na hatuna budi kujipanga upya ili kufanikisha malengo yetu kwenye michezo ijayo.
Ujumbe aliothibitisha kupokea tuhuma za baadhi ya mashabiki aliouandika kwenye ukurasa wake wa Twitter umesomeka hivi: “Nimepata meseji na comment kutoka kwa watu kadhaa kuwa hawajaelewa kiwango nilichoonesha ktk mechi za timu ya taifa, anyway ukweli nimefurahi kuona watu wanasema ukweli sichukii binafsi bali nachukuliwa km chachu itakayonifanya nijitume zaidi ili niwe bora zaidi, HAINA KUFELI.”
Samatta alifunga bao la kuongoza kwa njia ya mkwaju wa penati katika mchezo dhidi ya Libya, baada ya mshambuliaji Simon Msuva kuangushwa katika eneo la hatari kipindi cha kwanza.