Nahodha na Mshambuliaji wa Timu ya Taifa ya Tanzania ‘TAIFA STARS’ Mbwana Ally Samatta amewataka watanzania kufika kwa wingi Uwanja wa Benjamin Mkapa baadae leo Jumatano (Juni 08), kwa ajili ya kutimiza wajibu wao wa Kizalendo.
Taifa Stars leo itaikabili Algeria katika mchezo wa Mzunguuko wa pili wa ‘Kundi F’ wa kuwania kufuzu Fainali za AFCON 2023, baada ya kulazimisha sare ya 1-1 dhidi ya Niger Jumamosi (Juni 04) ugenini.
Samatta amesema wanafahamu nguvu ya Mashabiki wanapokua uwanjani na kuwashangilia, hivyo hana budi kuwaita na kuwataka kufanikisha sehemu ya lengo walilojiwekea kama wachezaji kwenye mchezo dhidi ya Algeria.
Hata hivyo Mshambuliaji huyo amesema wamejiandaa kikamilifu kupambana kwa dakika zote 90, na wana matarajio makubwa ya kuchota alama tatu za mchezo huo, ili kujiweka katika mazingira mazuri ya kuendelea kusaka tiketi ya kucheza AFCON 2023, kule Ivory Coast.
“Ni mchezo muhimu ambao ni wa kwanza kwetu nyumbani na tunahitaji alama tatu, kwa hiyo tutapambana kwa hali na mali ili tushinde.
“Tunajua mpinzani tunayekutana naye ni moja ya timu bora na kubwa Barani Afrika, lakini bado haitupunguzii morari ya kwenda kupambana nayo, ili kutimiza lengo letu.”
“Nawaomba watanzani waje Uwanja wa Mkapa kuja kutupa nguvu, na sisi kwa uwezo na umoja wetu tutakakikisha tunapambana kwa ajili yao ili tupate ushindi.”
Hadi sasa Algeria inaongoza msimamo wa ‘Kundi F’ ikiwa na alama tatu zilizotokana na ushindi wa 2-0 dhidi ya Uganda, huku Stars na Niger zikifuatia kwa kuwa na alama moja, na The Cranes inaburuza mkia wa kundi hilo.