Nahodha na Mshambuliaji wa Taifa Stars, Mbwana Samatta na wachezaji wenzake wa PAOK wapo kwenye hesabu za kupigania nafasi ya kucheza hatua ya makundi ya Europa Conference Ligi ambayo imetanguliza mguu mmoja ndani.
Ushindi wa mabao 2-1 ambao PAOK iliupata wiki iliyopita ikiwa Scotland dhidi ya Heart of Midlothian umeifanya kutanguliza mguu huo, chama hilo la Samatta linahitaji ushindi au sare ya aina yoyote ikiwa nyumbani wiki hii kwenye uwanja wao wa Toumba.
Kocha wa PAOK, Razvan Lucescu alisema kile ambacho kimetokea Scotland ni sehemu ya kwanza tu ya mchezo.
“Lazima tuwe makini sana katika mchezo unaofuata. Ninahisi lilikuwa pambano gumu, tuliweza kujibu staili ya Hearts na kuchukua fursa ya ubora wetu. Ninaamini tumepata matokeo ambayo tumestahili, hata kama yalikuwa magumu.”
Na jambo muhimu ni kwamba PAOK ya Ugiriki sio timu ya kinyonge katika michuano hiyo kwani msimu wa 2021-22 ilifika hatua ya robo fainali ambako iling’olewa na Marseille ya Ufaransa kwa matokeo ya jumla (3-1).
Kama PAAOK itatinga hatua ya makundi, Samatta ataweka rekodi ya kuwa mchezaji wa kwanza kutoka Tanzania na Afrika Mashariki kucheza michuano yote mitatu ya Ulaya.
Ikumbukwe nahodha huyo wa Taifa Stars tayari amecheza Ligi ya Mabingwa Ulaya, Europa Ligi akiwa na KRC Genk ya Ubelgiji na sasa anapigania nafasi ya kucheza Europa Conference Ligi.