Nahodha na mshambuliaji wa timu ya taifa ya Tanzania (Taifa Stars) Mbwana Samatta amesema wapo tayari kuanza harakati za kusaka nafasi ya kushiriki fainali za mataifa ya Afrika (AFCON 2021) dhidi Guinea ya Ikweta kesho Ijumaa.
Taifa Stars imedhamiria kushiriki kwa mara ya pili mfululizo fainali za mataifa ya Afrika, baada ya kufanikisha lengo mwaka huu 2019 na kuwa sehemu ya timu 24 zilizoshiriki fainali hizo nchini Misri.
Samatta amesema kwa muda wa siku nne sasa wachezaji wote wamekua katika ari ya kujifua mazoezini, na kila mmoja ameonyesha kuwa kwenye hatua nzuri ya kupambana dhidi ya wapinzani.
“Tupo tayari kwa mapambano, ninaamini kila mmoja kati yetu amejiandaa vyema kwa kufuata maelekezo ya benchi la ufundi ambalo limekua nasi bega kwa bega, tangu tulipoingia kambini mwanzoni mwa juma hili,” Amesema Samatta.
“Benchi la ufundi limefanya kazi kubwa ya kutuandaa kimwili na kiakili kabla ya kuwakabili Guinea ya Ikweta kesho Ijumaa, kazi imebaki kwetu kama wachezaji ili kufikia lengo, ambalo kila mtanzanai anatamani kuliona linatimia kwenye uwanja wa nyumbani kesho Ijumaa.”
“Ni haki kwa kila mtanzania kuja uwanjani kutushangilia na kutupa nguvu ya kuwakabili wapinzani wetu, ambao nina imani nao wamejiandaa vya kutosha kukabiliana na Taifa Stars, lakini hatuna budi kuitumia nafasi ya kucheza nyumbani na kupata alama tatu muhimu.”
Kwa upande wa kocha mkuu wa Taifa Stars Etienne Ndayiragije, ameonyesha kujiamini kuelekea mchezo wa kesho, kwa kusema hana shaka na kikosi chake, huku akiamini kitapambana na kupata matokeo mazuri dhidi ya wageni.
“Lengo ni kuanza vizuri mchakato wa kusaka nafasi ya kuelekea kwenye fainali zijazo za Afrika (AFCON 2021), nina matarajio makubwa ya kuwaona vijana wangu wakipambana bila kuchoka, ili kukamilisha lengo ya kufanya vizuri kwenye uwanja wa nyumbani. Kwa ujumla wachezjai wote wameonyesha kuwa na ari ya kupambana, na hilo nimeliona tukiwa katika maandalizi tangu walipoingia kambini mwanzoni mwa juma hili.” amesema kocha huyo kutoka Burundi.
Mchezo wa Tanzania (Taifa Stars) dhidi ya Guinea ya Ikweta umepangwa kuunguruma kuanzia mishale ya saa moja jioni, Uwanja wa Taifa Dar es salaam.
Michezo mingine ya kuwania kufuzu fainali za Afrika itakayounguruma leo.
Kundi A
Mali Vs Guinea
Kundi C
Ghana Vs South Africa
Kundi D
DR Congo Vs Gabon
Kundi F
Msumbiji Vs Rwanda
Kundi G
Egypt Vs Kenya
Togo Vs Comoros
Kundi H
Algeria Vs Zambia