Nahodha na Mshambuliaji wa timu ya taifa ya Tanzania Taifa Stars’, Mbwana Samatta, amesema kikosi chao kipo fiti kupata ushindi dhidi ya Niger katika mchezo wa Kundi F kuwania kufuzu Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON 2023).

Taifa Stars inayonolewa na Kocha Mualgeria, Adel Amrouche kitachuana na Niger kesho saa 10:00 jioni katika Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.

Katika Kundi hilo linaloongozwa na Algeria yenye alama 12 katika michezo minne, Taifa Stars inashika nafasi ya pili ikiwa na alama nne sawa na Uganda inayoshika nafasi ya tatu wakati Niger inaburuza mkia ikiwa na alama mbili.

Samatta amesema kikosi chao kimejiandaa vizuri ili kushinda mchezo huo na kujiweka katika nafasi nzuri ya kuwania kufuzu AFCON 2023.

“Kwa upande wetu sisi wachezaji tupo vizuri, tunaendelea na mazoezi kama kawaida kikubwa tunahamasishana kuhakikisha tunapata matokeo mazuri, maana ni mchezo wa mwisho kucheza nyumbani, kabla ya kwenda Algeria kumaliza michezo hiyo ya kuwania kufuzu.

Samatta amesema wachezaji wote wana imani kuwa, mbinu za kocha Amrouche, zitawasaidia kushinda mechi hiyo muhimu.

Hata hivyo Mshambuliaji huyo anayekipiga KRC Genk ya Ubelgiji, amewaomba Watanzania kujitokeza kwa wingi katika mchezo huo kuwaunga mkono ili waweze kupata nafasi ya kushiriki AFCON 2023.

Baada ya mchezo wa kesho Jumapili (Juni 18), Tanzania itabakisha mchezo dhidi ya Algeria utakaopigwa Septemba 4, mwaka huu nchini Algeria.

Amri Said: Nasreddinne Nabi ametuachia somo
Young Africans yaitega Azam FC kwa Fei Toto