Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan ameridhia wanafunzi 28,000 waliokidhi vigezo vya kupata mikopo ya elimu ya juu kwa mwaka 2022/2023 waende vyuoni kuendelea na usajili chini ya uratibu wa Wizara ya Elimu wakati taratibu muhimu zikikamilishwa.
Kauli hiyo imetolewa na Waziri Mkuu Kassim Mjaliwa hii leo Novemba 11, 2022 Bungeni jijini Dodoma wakati akiahirisha mkutano wa tisa wa Bunge la 12 hadi Januari 31, 2022 na kusema Lengo la Rais Samia ni kuwanufaisha wanafunzi wote wenye uhitaji.
Amesema, “Lengo la Mheshimiwa Rais ni kuwanufaisha wanafunzi wote wenye uhitaji, waliopata udahili na wenye vigezo vya kupata mikopo. Katika mapitio ya bajeti ya nusu mwaka baadaye mwaka huu tutaliomba Bunge lako tukufu liridhie matumizi ya fedha zitakazohitajika.”
Aidha, Majaliwa pia amewashukuru Wabunge kwa kuibua hoja zenye lengo la kuboresha utendaji wa Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu pamoja na mfumo mzima wa ugharamiaji, upangaji, utoaji na urejeshaji wa mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu nchini.
Amesema, miongoni mwa masuala yaliyojadiliwa kwa hisia na kupewa uzito mkubwa na Waheshimiwa Wabunge wakati wa mkutano huo ni hoja ya ugharamiaji, upangaji, utoaji na urejeshaji wa mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu.