Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan amesema mema yote yaliyoachwa na aliyekuwa Rais wa Awamu ya Tano, Hayati John Magufuli yataendelezwa, ambapo ametaja mambo hayo kuwa ni pamoja na nidhamu, uadilifu na kupiga vita ubadhilifu.
Rais Samia ameyasema hayo wakati wa maadhimisho ya mwaka mmoja wa kumbukizi ya kifo cha Hayati Magufuli.
“Hivi karibuni tutafungua daraja la Tanzanite lililoko jijini Dar es salaam hii ilikua ndoto ya Magufuli na nitaiendeleza kwa kuboresha huduma za maji, umeme na miundombinu”amesema Samia.
Ameelezea miradi iliyopo Geita ambapo amesema mradi wa kivuko cha Chato-Nkome kilichogharimu Sh3.1 bilioni umekamilika huku mradi wa kituo kikuu cha mabasi unaojengwa kwa Sh13.2 bilioni umesema umekamilika kwa asilimia 92 na kuahidi kuendelea kutoa fedha ili ukamilike kwa asilimia 100
Awali Makamu wa Rais wa Tanzania, Dkt. Philip Mpango amesema Magufuli alikua mwalimu wake aliyemfundisha kumtegemea Mungu nyakati za shida.