Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amewaagiza Wadau wote nchini kutoa ushirikiano wa hali ya juu katika kuhifadhi na kulinda ikolojia ya bonde la mto Ruaha Mkuu.
Ameyasema hayo mapema hii leo wakati wa uzinduzi wa kikosi kazi cha kuokoa ikolojia ya Bonde la mto Ruaha Mkuu iliyofanyika Mjini Iringa.
Amesema kuwa kwa miaka ya hivi karibuni mto huo ulianza kukakuka na hivyo kuwa katika hatari kubwa ya kutoweka na kuhatarisha hali ya uchumi wa Nchi na maisha ya mamilioni ya Watanzania wanategemea bonde la mto huo katika shughuli mbalimbali.
Aidha, amesema kuwa kutokana na matatizo mengi yanayokabili usimamizi wa hifadhi ya mazingira ya mto, baadhi ya matatizo hayo ni uharibifu wa misitu unaosababishwa na kilimo kisicho endelevu.
”Tumekutana hapa kwa lengo la kuzindua kikosi kazi hiki na kupitisha mpango kazi na kuwapa muongozo wa kuifanya kazi hii kwa weledi , ufanisi, uzalendo na maslahi mapana ya Nchi,” amesema Samia Suluhu.
Ameongeza kuwa jukumu kubwa la kikosi hiko ni kuharakisha na kurahisisha utekelezaji wa sera, sheria,Mikakati na Mipango ya hifadhi ya mazingira Serikali iliyojiwekea, na kusistiza kuwa hifadhi ya mazingira na matumizi bora ya rasilimali zake ndio msingi wa maendeleo endelevu na wajibu wa kila mmoja.
Hata hivyo, tofauti na uzinduzi huo, Makamu wa Rais hapo kesho anatarajia kutembelea bonde la Mto Ruaha Mkuu kwa ajili ya kujionea uharibifu wa Mazingira.