Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan amewataka chama cha wanasheria wanawake (TAWLA) wawasaidie wanawake wajasiriamali kujua sheria.
Bi. Samia ameyasema hayo leo wakati wa ufunguzi wa mkutano mkuu wa 28 wa Chama cha Wanasheria Wanawake Tanzania (TAWLA) uliofanyika katika hotel ya Serena jijini Dar es Salaam.
“Nawapongeza TAWLA kwa namna ya kipekee sana kwa kutimiza miaka 28 ya uhai wake. Ni miaka 28 ya mafanikio makubwa sana. Nawapongeza kwa sababu, katika miaka 28 ya uhai wenu, hamjawahi kuyumba wala kutoka nje ya lengo la kuanzishwa kwenu, ambalo ni kutumia taaluma ya sheria kuwasaidia wanawake wasio na uwezo kupata msaada wa kisheria na haki zao.” alisema makamu wa rais.
Makamu wa Rais ameongeza kuwa anatambua na kuguswa na kazi nzuri inayofanywa na chama cha wanasheria Wanawake (TAWLA) hapa nchini ya kupigania haki za wanawake kwa kutumia taaluma ya sheria hivyo serikali itaendelea kuwapa ushirikiano.