Viongozi wa Mikoa mitatu inayopitiwa na Bonde la Hifadhi ya Mto Ruaha Mkuu wametakiwa kuhakikisha wanakabiliana na changamoto ya kilimo katika vyanzo vya maji vya Hifadhi hiyo pia kukabiliana na shughuli za kilimo zinzofanyika katika bonde hilo.
Hayo yamesemwa na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan mara baada ya kufanya ziara fupi ya kutembelea Hifadhi ya Bonde la Mto Ruaha Mkuu hivi karibuni.
Amesema kuwa viongozi ndio wenye jukumu kubwa la kuweza kuwa elimisha wananchi namna ya kutumia bonde hilo ili kuweza kuondokana na uharibifu wa aina yeyote unao endelea kujitokeza na kuleta athari kubwa.
“Nawaagiza mkabiliane na tatizo hili hasa la kilimo karibu na bonde hili kwani wananchi wamekuwa wakilima kiholela, hali ambayo inapelekea uharibifu mkubwa wa mazingira na kupoteza uhalisia wa bonde hili uliokuwepo tangu hapo awali,”amesema Samia Suluhu.
Aidha, Viongozi walioagizwa kukabiliana na tatizo hilo ni kutoka katika Mikoa ya Iringa, Njombe na Mbeya, hivyo wametakiwa kupanga mikakati endelevu itakayowasaidia wananchi kuondokana na shughuli za kilimo katika bonde hilo.
Pia Makamu wa Rais ametembelea bwawa la kufua umeme la Mtera na kukutana na Meneja wa Kituo hicho, John Sikauki ambapo amemweleza kuwa hali ya ufuaji umeme ni nzuri na ameipongeza Serikali kwa jitihada inazofanya za kuokoa Hifadhi ya Bonde la Mto Ruaha Mkuu, kwani hicho ndicho chanzo cha kuaminika cha uzalishaji umeme katika bwawa la Mtera.
Hata hivyo Sikauki ameongeza kuwa hali ya mitambo ya ufuaji iko vizuri na huwa inafanyiwa ukarabati wa mara kwa mara hali ambayo inaifanya kuwa imara zaidi.