Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amemwakilisha Rais Dkt. Magufuli katika Mkutano wa Dharura wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) ambao umefunguliwa rasmi leo na Mwenyekiti wa Jumuiya hiyo Mfalme Mswati III mjini Mbababe –Swaziland.

Mkutano huo, wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) wanatarajia kujadili mambo mbalimbali yanayolenga kuimarisha utendaji kazi wa Jumuiya hiyo hasa katika sekta za viwanda, elimu, miundombinu, mtangamano wa masoko, ulinzi na usalama pamoja na kuweka mfumo wa kushirikisha sekta binafsi katika ngazi zote za utekelezaji wa mipango ya maendeleo kwenye jumuiya hiyo.

Mwenyekiti wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini Mwa Afrika Mfalme Mswati III wa Swaziland amesema kuwa nchi wanachama wa jumuiya hiyo wanatakiwa kuimarisha mipango na mikakati inayolenga kuhakikisha wananchi wa nchi za jumuiya hiyo wanapata huduma bora za kijamii.

Aidha,amesema kuwa nchi wanachama wa SADC wakishirikiana kwa pamoja katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya Jumuiya hiyo anaamini kuwa tatizo la uhaba wa ajira na umaskini litapungua kwa kiasi kikubwa kwenye nchi hizo.

Hata hivyo, Ujumbe wa Tanzania katika ngazi ya Mawaziri unaongozwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt Augustine Mahiga akisaidiana na Waziri wa Viwanda na Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage pamoja na Waziri wa Viwanda, Biashara na Masoko wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Balozi Amina Salum Ali.

Katika ngazi ya Makatibu Wakuu ujumbe wa Tanzania unaongozwa na Balozi Aziz Mlima Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.

Video: Rais Dkt. Magufuli kuweka jiwe la msingi barabara za juu Ubungo (Flyover)
Madaktari 500 kutoka Tanzania kuokoa jahazi nchini Kenya