Mwanariadha Mtanzania Samir Sururu, ameshinda medali ya shaba katika mchezo wa kurusha tufe katika mashindano ya riadha ya vijana wenye umri chini ya miaka 18 barani Afrika.
Mashindano hayo yaliyoanza Aprili 27, mwaka huu Lusaka nchini Zambia, yanatarajiwa kumalizika leo.
Sururu aliibuka mshindi wa tatu katika mchezo huo baada ya kurusha tufe umbali wa mita 16.89 akipitwa na washiriki wawili kutoka Afrika Kusini na Misri.
Kocha wa timu ya taifa ya riadha, Alfredo Shahanga, alisema katika mashindano hayo Tanzania imeshinda medali mbili.
Amesema mbali na Sururu, Mtanzania mwingine aliyeshinda medali ni Mwanaamina Mkwayu.
Shahanga amesema pamoja na ushindani mkali, anaamini vijana wake leo watafanya vyema zaidi.
Katika michuano hiyo, Tanzania inawakilishwa na wanariadha ambao ni Said Hamad Ali, Alex Sezario, Mpaji Gipson, Nicodemus Joseph, Samir Mbaraka Sururu, Nasra Abdallah Abdallah, Siwema Julius, Berthet Evarist, Salma Charles, Gasisi Geagase Girihuda, Elia Clement, Said Ali, Benedicto Maritius, Hafidh Talib na Mwanaamina Hassan Mkwayu.