Kiungo Samir Nasri ametaka meneja wa klabu ya Man City Pep Guardiola asitupiwe lawama kuhusu kuondoka kwake kwa mkopo Etihad Stadium, saa chache kabla ya dirisha la usajili kufungwa usiku wa kuamkia jana.

Nasri aliondoka klabuni hapo na kujiunga na klabu ya Sevilla CF kwa mkopo kwa kigezo cha kushindwa kupata nafasi ya kucheza katika kikosi cha kwanza cha Man City, licha ya kutumika kama mchezaji wa akiba mwishoni mwa juma lililopita.

Kiungo huyo kutoka nchini Ufaransa, amemkingia kifua Guardiola alipofanyiwa mahojiano kwa mara ya kwanza katika kituo cha televisheni cha klabu ya Sevilla CF ambayo imekua na historia ya kipekee kwenye michuano ya Europa League.

Nasri amesema Guardiola hakutaka kumruhusu aondoke mjini Machester kwa kigezo cha kuona kiwango chake kinatosha kuwania nafasi ya kuingia kwenye kikosi cha kwanza, lakini hakukubaliana na ombi hilo na badala yake alitaka auzwe kwa mkopo.

Amesema anaamini maamuzi ya kuondoka Man City kwa makubaliano ya kujiunga na Sevilla CF kwa mkopo wa muda mrefu, kutamsaidia kurejesha kiwango chake kama ilivyokua zamani tofauti na engendelea kukaa Etihad Stadium.

Hata hivyo Nasri mwenye umri wa miaka 29, ametoa sababu za kuikacha Man city katika kipindi cha msimu huu, kwa kutanabaisha kwamba kwa sasa klabu hiyo ina wachezaji ambao wana kiwango cha hali ya juu na endapo angebaki angekua na kazi ya ziada ya kushindana hasa ikizingatiwa alikua nje kwa muda mrefu akiuguza majeraha ya goti.

Amesisitiza kuwepo katika kikosi cha Sevilla CF kutampa changamoto mpya ya kucheza kwa kujituma zaidi, ili atakaporejea Man city kwa msimu ujao awe katika kiwango cha kushindana na wachezaji wengine.

Nasri alijiunga na Man City akitokea Arsenal mwaka 2011 na tangu alipotua Etihad Stadium ameshacheza michezo 124 na kufunga mabao 18.

Roberto Martinez Azomewa Hadharani
Free State Stars Waachana Na Mrisho Ngassa