Aliyekua nahodha na mshambuliaji wa timu ya taifa ya Cameroon Samuel Eto’o ameendelea kudhihirisha bado yupo katika medani ya soka la ushindani, baada ya kukamilisha taratibu za kujiunga na klabu ya Qatar SC.
Eto’o mwenye umri wa miaka 37 amejiunga na klabu hiyo inayoshiriki ligi kuu ya soka nchini Qatar, baada ya kuachwa na klabu ya Konyaspor ya Uturuki mwishoni mwa msimu uliopita.
Jana Jumatatu, Eto’o alithibitisha kuwa katika mazungumzo na baadhi ya timu zinazoshiriki ligi ya Ufaransa (Ligue 1), lakini mpango huo haukufanikiwa na badala yake ameibukia nchini Qatar.
Vyombo vya habari vya Qatar vilitoa taarifa za mshambuliaji huyo kwa bashasha kubwa, na inaaminika kwenda kwake nchini humo kutaendelea kuitangaza ligi yao.
Mchezo wa kwanza kwa mshambuliaji huyo unatarajiwa kuwa Ijumaa ambapo klabu yake ya Qatar SC itakua na jukumu la kuwakabili Al Sailiya katika uwanja wa Suhaim Bin Hamad.
Qatar SC inakua klabu ya 13 kwa Samuel Eto’o tangu aliupoanza kucheza soka la ushindani mwaka 1997 akiwa na mabingwa wa soka barani Ulaya Real Madrid.
Klabu nyingine alizowahi kuzitumikia ni Leganés kwa mkopo (1997–1998), Espanyol kwa mkopo (1999), Mallorca (2000-2004), FC Barcelona (2004–2009), Inter Milan (2009–2011), Anzhi Makhachkala (2011–2013), Chelsea (2013–2014), Everton (2014–2015), Sampdoria (2015), Antalyaspor (2015–2018) na Konyaspor (2018).