Nafasi ya Samuel Eto’o kama Rais wa Shirikisho la Soka Cameroon (FECAFOOT) ipo matatani baada ya Shirikisho la Soka Duniani (FIFA) kushinikizwa na kundi la maafisa wa soka nchini humo kumchukulia hatua Eto’o kutokana na masuala kadhaa ya kutatanisha likiwemo sakata la upangaji matokeo.
Kundi hilo ambalo ni pamoja na Rais wa Ligi ya soka la kulipwa Nchini Cameroon, Pierre Semengue na aliyekuwa Makamu wa rais wa FECAFOOT, Henry Njalla Quan Junior kwa pamoja waliwasilisha barua kwa Rais wa FIFA, Gianni Infantino na Rais wa (CAF) Patrice Motsepe wakihoji kwanini Eto’o ameendelea kusalia kuwa Rais wa FECAFOOT licha ya kashfa zake za nje ya uwanja
Mapema mwezi Agosti, Shirikisho la Soka Afrika (CAF) lilifungua uchunguzi dhidi ya mwenendo usiofaa wa Eto’o baada ya rekodi ya sauti kuvuja ikimuhusisha mshambuliaji huyo wa zamani wa Barcelona Inter Milan na Chelsea na kashfa ya upangaji matokeo ambayo hata hivyo alikanusha vikali.
Akizungumzia rekodi hiyo Eto’o aliiambia Gazzetta dello Sport:- “Nilikuwa nikizungumza na rafiki ambaye anawekeza katika soka na anataka kuifanya klabu yake kuwa moja ya klabu bora zaidi nchini Cameroon. Nilimhakikishia tu kwa kusema kwamba ningefanya kila niwezalo ili kuepuka makosa yoyote ya waamuzi dhidi yake.”
Sambamba na rekodi hiyo, barua hiyo inaangazia kesi yake ya ukwepaji kodi, tukio lake lililozua gumzo wakati wa kombe la Dunia 2022 baada ya mechi kati ya Brazil dhidi ya Korea ambapo limvaa na kumpiga mpiga picha sambamba na mkataba wake wa udhamini na Kampuni ya michezo ya bahati nasibu ya 1XBET.
Barua hiyo imegusia kitendo cha Rais wa shirikisho la soka Uhispania (RFEF) kujiuzulu nafasi yake kutokana na tukio la kumbusu mchezaji Jennifer Hermoso ikitaja hatua hiyo kama mfano ambao Eto’o alitakiwa kuufuata huku ikieleza kushangazwa na ukimya wa FIFA na CAF licha ya malalamiko ya wadau wa soka kutoka Cameroon.