Taasisi ya Sanaa na Utamaduni Bagamoyo – TaSUBa, imetajwa kuwa ni kitovu cha mafunzo ya tasnia za Sanaa na Utamaduni, huku Serikali ikiendelea kutoa fedha za kuiboresha miundombinu yake na vifaa vya kufundishia na kujifunzia na kusisitiza juu ya matumizi ya sanaa kuwaunganisha Wananchi.
Hayo yamesemwa na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko alipomwakilisha Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika Kilele cha Tamasha la 42 la Kimataifa la Sanaa na Utamaduni Bagamoyo, lililoandaliwa na Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo kwa kushirikiana na TaSUBa Mkoani Pwani.
Amesema, “niwapongeze Wizara kwa kuitangaza nchi yetu kwa kupitia kazi mbalimbali za utamaduni, sanaa na michezo. Aidha nakupongeza Waziri na wafanyakazi wa Wizara yako kwa kazi kubwa mnayoifanya kila mwaka katika kuliandaa na kuliendesha Tamasha hili kwa kipindi cha miaka 42 sasa.”
Dkt. Biteko pia ameipongeza TaSUBa kwa kukuza utalii wa kiutamaduni na kuvutia utalii wa ndani na nje, huku akiitaka Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo kuwa na Mipango mkakati wa kuwasaidia wasanii ili kupitia sanaa waweze kunufaika kiuchumi na kuitangaza nchi.
Kwa upande wake, Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye amesema tamasha hilo limekua na mafanikio makubwa kwa Bagamoyo na mkoa wa Pwani. Amesema wadau wamejitokeza kwa wingi na kulifanya liwe tamasha bora nchini.
Naye, Katibu Mkuu Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo, Gerson Msigwa amesema, tamasha hilo ni fursa ya kutangaza utalii uliopo nchini kwa kuwakutanisha wadau kutoka ndani na nje ya nchi. Amesisitiza kuwa mwaka 2024 tamasha litakuwa kubwa kwa kuwaleta wadau wengi zaidi nchini.
Wengine walioshiriki kilele cha tamasha hilo ni Mkuu wa Chuo TaSUBa, Dkt.Herbert Makoye, Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Abubakar Kunenge, Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo, Halima Okash, Watendaji wa Taasisi za Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo na Wadau wa Sanaa na Utamaduni.