Mfuko wa Utamaduni sanaa Tanzania, umetoa wito kwa Wasanii wenye sifa za kupata mkopo kutoka katika taasisi hiyo, kujitokeza kuwezeshwa fedha au Vifaa vitakavyo wasaidia kuboresha kazi zao za Sanaa, ili kuendana na soko la sasa.
Wito huo, umetolewa na Mtendaji Mkuu wa Mfuko huo, Nyakango Mahemba ambaye amesema hatua hiyo imelenga kutoa mikopo yenye Masharti nafuu kwa Msanii mmoja mmoja, Vikundi au Makampuni yanayotengeneza kazi za sanaa inayoanzia Shilingi laki 2 Mpaka milioni 100, huku riba ya Mkopo huo ikiwani ni asilimia 9 inayotozwa katika salio la Mkopo.
Amesema, ”ili mtu anufaike na mikopo yetu ni lazima awe Tanzania,awena umri kuanzia miaka 18 na kuendelea, afanye kazi za utamaduni pamoja na Sanaa na vilevile anatakiwa ajisajili katika taasisi ya BASATA ambao wao ndiyo wapo kisheria katika kusimamia kazi za Sanaa pia Mwombaji anapaswa kuandika andiko la Miradi itayo elezea madhumuni na malengo ya mkopo wake.”
Kwa upande wake Msanii wa Nyimbo za Muziki wa Kisasa ‘Bongo Fleva’, Masinde Badi kutoka mkoa wa Manyara pamoja na wasanii waliofikiwa na kuelimishwa juu ya umuhimu wa mfuko wa utamaduni na sanaa, wameishukuru Serikali kwa kubuni na kuanzisha mfuko huo kwani utawasaidia kuongeza ufanisi na ubora wa kazi za sanaa nchini.
Mikopo hiyo inayotolewa na Mfuko wa Utamaduni sanaa Tanzania, imegawanyika katika aina tano ikiwa ni pamoja na Sanaa za Ufundi, Sanaa za Maonesho pamoja Sanaa za Muziki.