Klabu ya Everton imekamilisha mpango wa kumsajili mshambuliaji hatari wa Malaga CF ya Hispania, Sandro Ramirez mwenye umri wa miaka 21.
Kwa mujibu wa gazeti la The Express, Everton imefanikiwa kumsajili mshambuliaji huyo wa zamani wa FC Barcelona licha ya kuwepo kwa taarifa kuwa Atletico Madrid ilijaribu kutibua dili hilo katika dakika za mwisho kwa kutaka kupanda dau.
Lakini adhabu ya kufungiwa kusajili iliyotolewa na FIFA dhidi ya klabu hiyo ya mjini Madrid ilifuta mpango huo.
Usajili wa mshambuliaji huyo aliyeifungia Malaga mabao 14 na kupika mengine matano katika michezo 30 ya ligi ya La Liga msimu uliopita, unadaiwa kuigharimu Everton kiasi cha Pauni milioni 5.25.
Ramirez aliyejiunga na Malaga CF msimu uliopita baada ya kutupiwa virago na FC Barcelona amejiunga na Everton kwa mkataba wa miaka mitano na atakuwa akivalia jezi namba tisa (9).
Ramirez anakuwa mchezaji wa nne kujiunga na Everton katika kipindi hiki cha usajili barani Ulaya. Wengine ni Jordan Pickford, Davy Klaassen na Henry Onyekuru.