Klabu ya Newcastle United imemsajili kiungo wa kati wa AC Milan na Italia, Sandro Tonali kwa uhamisho wa ada ya pauni milioni 55 (Sh bil 168.3).

Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 23, ametia saini kwenye mkataba wa miaka mitano na kuwa usajili wa kwanza kwa Kocha Eddie Howe msimu huu wa joto huku timu yake ikijiandaa na Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Ada iliyoripotiwa ya pauni milioni 55 inamfanya kuwa mwanasoka ghali zaidi wa Italia wakati wote.

Tonali aliisaidia AC Milan kushinda Serie A msimu wa 2021-22 na alikuwa sehemu ya timu iliyofika nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa msimu uliopita. Pia alikuwa kwenye kikosi cha Italia kwenye mashindano ya Ulaya ya U-21.

Tonali aliiambia tovuti ya klabu kuwa: “Nataka kulipa imani yangu uwanjani, nikifanya yote niliyokuwa nayo siku zote.

Nina furaha sana kucheza katika uwanja wa St. James Park, siwezi kusubiri kuhisi joto la mashabiki.”

Kocha mkuu wa Newcastle Howe alisema kuhusu Tonali: “Ana kipaji cha kipekee na ana akili, umbile na sifa za kiufundi za kutufaa sana.

Akiwa na umri wa miaka 23, Sandro tayari ana uzoefu, ni mchezaji muhimu katika mojawapo ya ligi kuu za Ulaya na Ligi ya Mabingwa, na pia kuichezea nchi yake.

“Lakini pia ana nafasi na uwezo wa kukua na kubadilika na sisi, ninafuraha kumuongeza kwenye kikosi chetu tunapokaribia msimu ujao.”

Rais Chakwera ampokea Balozi Kayola
Habari Kuu kwenye magazeti ya leo Julai 6, 2023