Aliyekua Mkurugenzi wa klabu ya Singida United Festo Sanga, ameutaka uongozi wa Young Africans kujipanga kwa msimu ujao wa Ligi Kuu Tanzania Bara, ili kufikia lengo la kutwaa ubingwa wa ligi hiyo.

Festo Sanga ambaye kwa sasa ni mbunge Jimbo la Makete, ametoa ushauri huo kwa uongozi wa Young Africans, kufuatia kuona Simba SC ina nafasi kubwa ya kutetea taji la VPL kwa msimu wa nne mfululizo.

Sanga amesema: “Simba SC inabeba ubingwa wa VPL, Young Africans inapoteza muda tu, kwa sababu wameingia kwenye malumbano ya wao kwa wao. Wamefukuza benchi zima la ufundi hadi kocha msaidizi waliyemwajiri jana wakamfukuza kesho yake.”

“Kufukuza benchi la ufundi bado sio suluhisho, wanatakiwa kukaa chini kuangalia tatizo. Wachezaji sio tatizo, wanawachezaji wazuri tatizo wanacheza huku wanamwangalia aliye nyuma yao.”

“Simba SC inabidi tuwapongeze kuanzia uongozi, wamewekeza na wanatakiwa kuwa darasa kwa wangine kwamba ukiwekeza kwenye mpira inalipa.”

“Kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu Simba itafika mbali kwa sababu ina kikosi imara.”

Licha ya Sanga kuiondoa Young Africans kwenye ubingwa wa VPL msimu huu, bado klabu hiyo kongwe katika ukanda wa Afrika mashariki na kati inaendelea kuongoza msimamo wa Ligi Kuu kwa kuwa na alama 50, huku ikicheza michezo 23.

Simba SC inashika nafasi ya pili kwenye msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara ikiwa na alama 46, huku ikicheza michezo 20, na Azam FC inashika nafasi ya tatu kwa kufikisha alama 44 na kucheza michezo 24.

Bunge laipongeza Simba SC
Msumbuji yahitaji msaada wa kigeni kupambana na uasi