Kocha aliekatisha furaha ya majogoo wa jiji Liverpool usiku wa kuamkia leo katika mchezo wa ligi ya mabingwa barani Ulaya, Eduardo Berizzo amegundulika kuwa na tatizo la saratani la kibofu.

Klabu ya Sevilla inayotumikiwa na kocha huyo kutoka nchini Argentina, imethibitisha taarifa hizo za kitabibu mapema leo asubuhi.

Taarifa za Berizo mwenye umri wa miaka 48, zilianza kusikika kama tetesi wakati wa mapumziko katika mchezo wa jana, ambapo kikosi chake kilikua nyuma kwa mabao matatu kwa sifuri, kabla ya vijana wake hawajarejea uwanjani na kusawazisha mabao hayo na kuufanya mchezo kumalizika kwa matokeo ya sare.

Mabao ya Liverpool yalifungwa na Roberto Firmino aliyefunga mawili, na Sadio Mane.

“Taarifa ya idara ya tiba ya Sevilla FC ni kwamba kocha wa timu ya kwanza, Eduardo Berizzo amekutwa na tatizo ya saratani ya kibofu.

Vipimo zaidi vitaamua hatua inayofuata ya matibabu. Sevilla FC inataka kuonyesha sapoti kamili kwa kocha wake kwa sasa na inamtakia kupona haraka.” Imeeleza taarifa za klabu.

Guido Pizarro aliifungia Sevilla bao la tatu la kusawazisha dakika ya tatu ya muda wa nyongeza baada ya kutimia dakika 90 za kawaida katika mchezo wa jana na wachezaji wote wakamkimbilia Berizzo kushangilia naye. Mabao mengine ya Sevilla yalifungwa na Yassim Ben Yedder.

Inafahamika Muargentina huyo ambaye aliisaidia Celta Vigo kufika Nusu Fainali ya Europa League msimu uliopita, atakwenda kufanyiwa matibabu baadae.

Msibadili tukio la Lissu kuwa mtaji wa siasa- Nchemba
Kivumbi cha ligi ya mabingwa kuendelea leo