Mfalme wa Saudi Arabia, Salman bin Abdulaziz Al Saud amepiga marufuku watu kutoka nje kuanzia saa moja jioni hadi saa kumi na mbili asubuhi, ikiwa ni mkakati wa kudhibiti mlipuko wa virusi vya Corona.
Wanaofanya kazi katika sekta ya afya, vyombo vya habari, Jeshi na vyombo vya usalama wameruhusiwa kuendelea na majukumu yao. Watu wengine wametakiwa kubaki nyumbani isipokuwa pale wanapokuwa na sababu za msingi.
Agizo hilo la siku 21 linaanza kutekelezwa leo na watakaoruhusiwa kutoka nyumbani ni wafanyakazi kutoka sekta binafsi na za umma ambao huduma zao zinahitajika katika kupambana na Virusi hivyo.
Kwa mujibu wa Wizara ya Afya, idadi ya maambukizi nchini humo imeongezeka na kufikia 511 baada ya wagonjwa 119 kuripotiwa Jumapili ambapo 72 kati yao ni raia wa Uturuki waliowekwa karantini katika mji Mtakatifu wa Makkah.
Msemaji kutoka Wizara hiyo, Mohammed Abdelali amesema watu 23,000 wamepimwa COVID-19 nchini humo hadi sasa na 17 wameruhusiwa kutoka Hospitali baada ya kupona.