Saudi Arabia imekanusha vikali ripoti ya kijasusi iliyotolewa na Marekani ikifichua kuwa mrithi wa kiti cha ufalme wa nchi hiyo Mohammed bin Salman aliidhinisha mauaji ya mwandishi habari Jamal Khashoggi mwaka 2018.
Taarifa iliyotolewa na Wizara ya Mambo ya Kigeni ya Saudi Arabia imesema serikali mjini Riyadh inaipinga vikali ripoti hiyo ikisema imejaa taarifa za uzushi na tathmini isiyokubalika kuhusu utawala wa falme hiyo ya eneo la Ghuba.
Tathmini hiyo ya Marekani iliyotolewa na utawala wa rais Joe Biden kutoka ripoti pana ya kijasusi imehitimisha kuwa Bin Salman aliidhinisha operesheni ya kumkamata au kumuua Khashoggi mjini Istanbul, nchini Uturuki.
Hapo kabla Saudi Arabia ilisema mauaji ya Khashoggi kwenye ubalozi mdogo wa Saudi Arabia nchini Uturuki, yalifanywa katika operesheni ya kihalifu na kukanusha kuhusika kwa mwanamfalme Salman.
“Kwa bahati mbaya kuwa ni kweli kwamba ripoti hii, ikiwa na hitimisho lisilo sahihi, imetolewa wakati falme hii imekwisha kosoa uhalifu huo wa kutisha, na uongozi wa Saudia ulichukua hatua zinazohitajika kuhakikisha kisa kama hicho hakitokei tena,” imesema sehemu ya taarifa ya Wizara hiyo ya Mambo ya Kigeni.
Taarifa hiyo pia imeongeza kusema Saudi Arabia inapinga kile imekiita uingiliaji wa utawala wake na uhuru wa mfumo wake wa kutoa haki.
Kwa mujibu wa ripoti ya Marekani, kutokana na ushawishi wa mwanamfalme Salman siyo rahisi kuwa mauaji ya Khashoggi yalitokea bila kuyaidhinisha.
Jamal Khashoggi aliyekuwa uhamishoni Marekani akiandika ripoti zinazomkosoa Mohammed Salman na serikali ya Saudi Arabia, aliuawa tarehe 2 mwezi Oktoba mwaka 2018.
Mwandishi huyo aliyekuwa na umri wa miaka 59 wakati wa mauaji yake, aliambiwa na balozi wa Saudia afike katika ubalozi wa taifa hilo mjini Istanbul, ili kupata nyaraka kadhaa alizohitaji ili aweze kufunga ndoa na mpenzi wake raia wa Uturuki, Hatice Cengiz.
Mwezi mmoja baada ya mauaji hayo, shirika la Ujasusi la Marekani, CIA lilisema kwa kujiamini kuwa mrithi wa kiti cha ufalme wa Saudi Arabia, Mohammed bin Salman, ndiye aliyeamuru mauaji hayo, madai ambayo Bin Salman aliyakanusha.
Mrithi huyo wa kiti cha ufalme, Mohammed bin Salman, ameendelea kukanusha kuhusika na mauaji hayo hata baada ya washauri wake wa karibu kutiwa hatiani na mamlaka za sheria nchini mwake kwa kuhusika nayo.
Kufuatia kutolewa kwa ripoti hiyo, Waziri wa Mambo ya nchi za nje wa Marekani, Antony Blinken amesema Washington inalenga kuchukua mwelekeo mpya wa kisera lakini siyo kuvuruga mahusiano yake na Saudi Arabia ambayo ni mshirika wa karibu wa usalama kwenye eneo la Mashariki ya Kati.
Licha ya hasira iliyoelezwa na Saudi Arabia, nchi hiyo imesisitiza nia yake ya kuendeleza uhusiano na Marekani.
“Ushirika baina ya Marekani na Saudi Arabia ni imara na stahamilivu” imesema taarifa kutoka Saudia.