Baadhi ya Wachezaji wa Simba SC akiwemo kiungo mshambuliaji kutoka Ghana Augustine Okrah wamepewa dakika 180 kuonyesha makeke yao kabla ya panga kubwa kupita kwa ajili ya kusuka upya kikosi kitakachokuwa na ushindani ndani ya 2023/24.

Miongoni mwa mastaa ambao wanatajwa kuwa kwenye uangalizi mkubwa ni pamoja na beki wa kazi Joash Onyanga, Okrah, Gadiel Michael, Habib Kyombo pamoja na Ismail Sawadogo.

Nyota hawa wanatajwa kuwa kwenye hesabu za kupewa mkono wa kwaheri ikiwa hawatafikia malengo yaliyowekwa pamoja na sababu za viwango vyao kuwa vya kupanga na kushuka.

Meneja wa Idara ya Habari na Mawasiliano Simba, Ahmed Ally amesema kuwa kwa sasa kinachosubiriwa ni ripoti ya Kocha Mkuu, Roberto Oliveira ‘Robertinho’.

“Kwa sasa ripoti bado haijatolewa na kinachosubiriwa ni kukamilisha kwa msimu ukizingatia kwamba tuna mechi mbili zimebaki zote ni muhimu. Tukishamaliza hapo tutaanza kufaya usajili.

“Mechi hizi tutakuwa nyumbani baada ya mechi hizi kukamilika hapo tunaamini ripoti itakuwa tayari na Wanasimba watapata kile kilicho bora, wazidi kuwa pamoja nasi na wawe na subira,” amesema Ally

Mchezo ujao wa Simba yenye alama 67 ikiwa nafasi ya pili ni dhidi ya Polisi Tanzania unatarajiwa kuchezwa Uwanja Azam Complex, Juni 06.

Urusi yatangaza ushindi, Ukraine yaubeza kiaina
Expressway Kibaha - Chalinze - Moro ipo mbioni - Serikali