Shirikisho la soka nchini  (TFF) limemteua Sebastian Nkoma kuwa Kocha Mkuu wa timu ya soka taifa ya wanawake wa Tanzania Bara maarufu kwa jina la Kilimanjaro Queens ambayo kwa mara ya kwanza inakwenda kushiriki mashindano ya kuwania Kombe la Afrika Mashariki na Kati yatakayofanyika kwa siku tisa kuanzia Septemba 11, 2016 jijini Jinja, Uganda.

Uteuzi huo wa Nkoma unakwenda sambamba na wasaidizi wake, ambao ni Hilda Masanche na Edna Lema wakati Meneja wa timu hiyo, Furaha Francis. Mtunza vifaa ni Esther Chabruma maarufu kwa jina la Lunyamila.

Kabla ya uteuzi huo, Nkoma alikuwa Kocha Msaidizi wa timu ya Mpira wa Miguu ya Vijana wenye umri wa chini ya miaka 17 ‘Serengeti Boys’ ambayo kwa sasa ipo kambi ndogo ya kwenye hosteli za TFF kujiandaa na kambi kubwa itakayofanyika Shelisheli kabla ya kuivaa Congo – Brazzaville kwenye mchezo wa kuwania nafasi ya kucheza fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika kwa vijana wenye umri huo. Fainali hizo zitapigwa Aprili mwakani, nchini Madagascar.

Kilimanjaro Queens inatarajiwa kuanza mazoezi ya leo, Septemba mosi, 2016 ambako wachezaji watakuwa wanakwenda mazoezini Uwanja wa Karume, Ilala  na kurudi nyumbani hadi Jumapili ambako Jumatatu itasafiri kwenda Uganda kupitia Bukoba mkoani Kagera itakakoweka kambi tena ya siku nne. Septemba 8, mwaka huu itacheza mechi ya kirafiki dhidi ya Burundi ambayo pia itakuwa njiani kwenda Uganda kwenye mashindano hayo yanayoratibiwa na Baraza la Vyama vya Mpira wa Miguu Afrika Mashariki na Kati (CECAFA).

Kwa mujibu wa CECAFA, michuano hiyo itafanyika jijini Jinja na Tanzania ambayo inaongoza kwa ubora wa viwango vya Mpira wa Miguu kwa nchi za Afrika Mashariki imepangwa kundi B ikiwa pamoja na timu za Rwanda na Ethiopia wakati kundi A litakuwa na timu za Kenya, Burundi, Zanzibar pamoja na mwenyeji Uganda,.

Tanzania itafungua michezo hiyo kwa kucheza na Rwanda Septemba 12, 2016 kabla ya kucheza na Ethiopia Septemba 16, 2016. Rwanda na Ethiopia zitacheza Septemba 14, 2016 wakati kundi A Zanzibar itakata utepe kwa kucheza na Burundi na siku hiyohiyo, Uganda itacheza na Kenya.

Michezo mingine ya kundi A itakuwa ni kati ya Burundi na Kenya zitakazocheza Septemba 13, 2016 ambako siku hiyohiyo Zanzibar itacheza na Uganda. Septemba 15, Kenya itacheza na Zanzibar na Uganda itafunga hatua ya makundi kwa siku hiyo kwa kucheza na Burundi.

Nusu fainali itafanyika Septemba 18, kabla ya fainali kufanyika Septemba 20, 2016 ikitanguliwa na mchezo wa kusaka mshindi wa tatu na nne.

Mashindano ya CECAFA kwa timu za wanawake yanafanyika kwa mara ya kwanza jambo linaloleta tafsiri kuwa michuano hiyo inaweza kuinua soka la wanawake kwa ukanda wa Afrika Mashariki na Kati. Tanzania inatarajiwa kuanza kambi Septemba mwanzoni kwa mazoezi ya kwenda na kurudi nyumbani kwa wiki moja na baadaye wataingia kambini moja kwa moja tayari kwa safari ya Uganda.

Malinzi Ampongeza Rais Mpya Wa EFA
Magufuli agusia mpango wa kubadili ‘fedha’ kuwakomoa waliozificha