Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Hussein Kattanga amesema lengo la Serikali ni kuhakikisha sekta binafsi inawekeza katika sekta za mifugo na uvuvi ili wananchi waweze kunufaika zaidi kupitia fursa zilizopo katika sekta hizo.
Balozi Kattanga amebainisha hayo jijini Mbeya, na kudai kuwa Wizara inatakiwa kuhamasisha wananchi na wadau mbalimbali kuwekeza katika sekta za mifugo na uvuvi kwa kuwa zina tija zaidi kiuchumi.
Amesema, “Ni wakati kwa Wizara ya Mifugo na Uvuvi kuhakikisha inatoa elimu zaidi juu ya ufugaji wa mifugo na viumbe maji ili wananchi waweze kujikita katika sekta hizo ambazo ni rahisi katika kukuza kipato chao na uchumi wa nchi kwa ujumla.”
Kwa upande wake Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia Mifugo Tixon Nzunda amemwambia Katibu Mkuu Kiongozi kuwa, Wizara imekua kwenye kampeni ya nchi nzima kuhamasisha wafugaji kuiwekea mifugo yao hereni za kieletroniki ili iweze kutambulika na serikali kujua idadi ya mifugo na huduma mbalimbali ambazo zinatakiwa kwa wafugaji.
Amesema, licha ya changamoto mbalimbali ambazo wizara imekuwa ikikutana nazo za baadhi ya wafugaji kutoelewa vyema zoezi hilo na kutoonesha utayari wa kuwekea mifugo yao hereni, bado elimu imekuwa ikitolewa kwa kushirikiana na Chama cha Wafugaji Tanzania (CCWT).
Naye, Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia Uvuvi Dkt. Rashid Tamatamah amesema wizara tayari ipo katika hatua mbalimbali za ujenzi wa bandari ya uvuvi katika Wilaya ya Kilwa Mkoani Lindi ikiwa ni mojawapo ya matayarisho kwa ajili ya uvuvi wa bahari kuu.
Dkt. Tamatamah amebainisha kuwa, “uvuvi wa bahari kuu utaenda sambamba na uwepo wa meli zenye uwezo wa kuvua katika kina kirefu cha bahari pamoja na kuvutia sekta binafsi kushirikiana na serikali katika kufanikisha uvuvi huo.”