Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt .Dorothy Gwajima amekutana na kufanya mazungumzo na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Maendeleo la USWISI Patricia Danzi aliyeambatana na ujumbe kutoka Shirika hilo.
Katika kikao hicho kwa pamoja wamekubaliana kuendelea kuimarisha ushirikiano katika kuketa Maendeleo nchini hususan katika eneo la huduma za afya kwa Watanzania.
Dkt. Gwajima amesema, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Wizara ya Afya inaendelea kuboresha huduma za afya, na sasa ipo mbioni kupitisha sheria ya Bima ya Afya kwa wote itayomruhusu kila mwananchi kuwa na Bima ili kupata huduma za matibabu.
Amesema, kama nchi inaendelea kuimarisha mapambano dhidi ya ugonjwa wa Malaria kwa kupitia afua mbalimbali ikiwemo utoaji elimu kwa wananchi juu ya njia bora za kujikinga dhidi ya Malaria na ujenzi wa kuwanda cha viuadudu kilichopo Mkoa wa Pwani.
Aidha, Dkt. Gwajima amesema kuwa, Tanzania inaendelea na mapambano dhidi ya UVIKO-19 kupitia afua ya Elimu kwa wananchi juu ya njia bora za kujikinga dhidi ya UVIKO-19 na utoaji wa Chanjo ya UVIKO-19, huku akieleza tayari Tanzania imepokea Chanjo tofauti ikiwemo Jenseen, Sinopharm na Pfizer.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Maendeleo la USWISI Bi. Patricia Danzi amesema Serikali ya Uswisi imekuwa mdau mzuri wa mapambano dhidi ya UVIKO-19 kwa kuchangia zaidi ya Dozi 4,000,000 kupitia mpango wa COVAX Facility ambapo Tanzania ni moja ya wanufaika wa mpango huo.
Viongozi hao wamekutana leo, katika ofisi za Wizara ya Afya Jijini Dodoma na kikao hicho kimehudhuriwa na baadhi ya Maafisa kutoka Wizara ya Afya na Shirikishi la Maendeleo la Uswisi.