Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Othman Masoud Othman, amesema uchumi wa Zanzibar kupitia sekta ya Utalii, unachangia asilimia 29.2 ya Pato la Taifa kwa Zanzibar, ambazo hazifikiwi na sekta nyengine yoyote ya uzalishaj
Othman, ameyasema hayo mjini Zanzibar katika ufunguzi wa Kongamano la kuadhimisha siku ya Utalii Duniani, inayofanyika Septemba 27, ya kila mwaka.
Amesema, hatua hiyo itasaidia kwenda sambamba na maudhui ya kauli mbiu ya mwaka huu ya siku ya Utalii inayohimiza kuifikiria upya sekta ya Utalii ambayo imepita kipindi kigumu cha maradhi ya Uviko-19.
Aidha, ameongeza kuwa, utalii, ni Sekta mtambuka inayogemewa na sekta nyengine zote nchini, zikiwemo za ajira, miundombinu, nishati, uchumi wa buluu, na kilimo, na upatikanaji wa huduma za kijamii.
Hata hivyo, Othman amesema wakati umefika kwa Zanzibar kuacha kujitangaza kama ni kituo cha utalii cha Jua, Mchanga na Bahari pekee, bali itumie vivutio vya kiutamaduni, historia, vyakula, dini, na matibabu , ambavyo vinajipambanua na nchi nyengine kwa vile havipatikani popote duniani.
kongamano hilo, litachangia kuuamsha ‘ulimwengu wa kitalii’ kutokana na Zanzibar kuwa tayari kuwapokea watalii, muda wowote, sambamba na kutekeleza itifaki ya kudhibiti maambukizi ya Uviko-19 kwa ushirikiano na sekta binafsi.