Bondia wa ngumi za kulipwa wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Seleman Kidunda ameingia mkataba wa pambano dhidi ya Eric Mukadi raia wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo.
Pambano hilo lililoandaliwa na Kampuni ya ngumi za kulipwa ya PFA Promotion Entertainment, linatarajiwa kupigwa Juni 30, mwaka huu kwenye Ukumbi wa Mlimani City, Dar es salaam.
Pia pambano jingine siku hiyo linatarajiwa kuwa baina ya Mfaume Mfaume akizichapa na Nkululeko Mhlongo raia wa Afrika Kusini.
Akizungumza baada ya kumalizika kwa zoezi la kusaini mikataba kwa mabondia hao, Mkurugenzi wa PFA, Fadhili Maogola amesema wameamua kumchukua Kidunda kutokana na kutambua ubora wake wakiamini atatoa upinzani wa kutosha kwa mpinzani wake huyo.
“Tumempa mkataba Kidunda kwa ajili ya pambano letu la Hata Usipolala Patakucha Tu, yeye na Mfaume watapanda katika ulingo mmoja siku hiyo pale Mlimani City kuonesha ukali wao katika mapambano ambayo haya ya kimataifa maana hakuna asiyejua ubora wao.” amesema Maogola