Mahakama ya Wilaya ya Iringa, imemuhukumu kifungo cha maisha Jela, fidia ya Shilingi milioni 25, faini ya Shilingi milioni 5 na adhabu ya viboko 11 Selemani Gwabuka (78), mkazi wa Idodi baada ya kukutwa na hatia ya kosa la kubaka mtoto mwenye umri wa miaka 11 na kumuambukiza VVU, huku akijua yeye ni muathirika anayetumia dawa za kufubaza virusi – ARV.
Akisoma hukumu hiyo Hakimu Mkazi wa Mahakama hiyo, Said Ally Mkasiwa amesema mtuhumiwa huyo amekutwa na hatia hiyo bila kuacha shaka, kuwa alimbaka mtoto wa miaka 11 na kumuambukiza Virusi vya Ukimwi kwa makusudi.
Katika vielelezo vilivyowasilishwa Mahakamani hapo, vilionyesha kuwa mtuhumiwa Selemani aligundulika kuwa na virusi vya ukimwi mwaka 2016 katika Kituo cha Afya cha Mahuninga na alianza kutumia ARV.
Mbele ya Mahakamani, Mwendesha Mashtaka wa Serikali, Burton Mayage aliiomba Mahakama Kutoa adhabu kali Kwa mtuhumiwa kwani ugonjwa aliomuambikiza mtoto huyo hauna tiba na utadumu katika maisha yake, jambo litakalomuathiri kisaikilojia.