Kocha Msaidizi wa Mabingwa watetezi Tanzania Bara Simba SC Seleman Matola amesema bado kuna tatizo la kukosa umakini kwa wachezaji wa klabu hiyo wanapokua langoni mwa timu pinzani katika michezo ya Ligi Kuu.
Simba SC leo Alhamis (April 07), ilikua mgeni wa Coastal Union katika Uwanja wa CCM Mkwakwani jijini Tanga, huku ikiibuka na ushindi wa mabao 2-1.
Kocha Matola amezungumza kwa niaba ya Kocha Mkuu Franco Pablo Martin baada ya mchezo huo kimalizika, ambapo alisema kikosi chao kilikua na uwezo wa kupata mabao zaidi ya mawili.
Amesema walitengeneza nafasi nyingi za mabao kila walipofika langoni mwa Coastal Union lakini umakini ulikua mdogo na kujikuta wakipoteza nafasi za wazi.
“Tatizo la umakini limetugharimu, tulipaswa kupata zaidi ya mabao mawili kwa sababu tumetengeneza nafasi nyingi sana za mabao, tutaendelea kulifanyia kazi hili tatizo.”
“Kwa hatua nyingine niwapongeze wachezaji wa Simba SC kwa kupata ushindi, pia niwapongeze Coastal Union kwa mchezo mzuri uliotupa changamoto kwa wakati wote.” amesema Matola.
Simba SC walikuwa wa kwanza kupata bao dakika ya 39 likifungwa na Bernard Morrison baada ya beki wa Coastal kufanya uzembe ndani ya kumi na nane Morrison kuuwahi Mpira.
Kiungo Mkabaji kutoka Nigeria Victor Akpan aliisawazishia Coastal dakika ya 76 kwa shuti kali lililoenda moja kwa moja na kumuacha Aishi Manula.
Akitokea benchi Mshambuliaji hatari Meddie Kagera alipigilia msumari wa pili dakika ya 90+2 kwa bao safi huku Coastal walipata pigo dakika ya 87 kwa beki wake Patrick Kitenge kuonyesha kadi nyekundu.
Kwa ushindi huo Simba wamefikisha alama 40 zinazoiweka nafasi ya pili huku Coastal Union wakibaki nafasi ya 12 wakiwa na alama 21.